Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeshiriki kikamilifu katika kutoa maoni katika utengenezaji na uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ili kuhakikisha kuwa Dira hiyo inaakisi masuala yote ya Sekta ya Sheria.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezungumza hayo katika mahojiano maalumu na vyombo vya habari yaliyofanyika Ofisini kwake, Mtumba Jijini Dodoma, tarehe 10 Machi, 2025.

Amesema kuwa Ofisi yake imejipanga kuhakikisha kwamba mambo yote yanayoihusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanatekelezwa ipasavyo ili kuweza kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050.

“Sisi kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tutahakikisha kwamba tunaoanisha vizuri Sheria zetu tulizonazo na kule tunakotaka kwenda, ni lazima tuwe na legal framework ya kutufikisha.” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema suala la kufanya maboresho katika Sheria mbalimbali ziweze kuendana na mabadiliko ya Kijamii, kiuchumi pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria.

“Sisi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tunataka kuwa champion wa kuhakikisha kuwa sheria zetu zote tunazioanisha na Dira ya Taifa ya 2050,” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameongelea suala la ufasiri wa Sheria, ambapo amesema kwakua Sheria mbalimbali zimeweza kutasfiriwa kutoka lugha ya Kingereza kwenda Kiswahili kwakuwa ili ziweze kutumika kwa urahisi na watumiaji.

“Kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2024 tumeweza kutafsiri jumla ya Sheria kuu 300 lengo kubwa ikiwa ni kuwarahisishia watumiaji wa Sheria,”amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Sambamba na hilo, Johari amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeweza kukamilisha zoezi la Urekebu wa Sheria, ambapo Sheria mbalimbali zilizorekebishwa zimeweza kufanyiwa Urekebu, hivyo watumiaji wa Sheria watapata Sheria hizi zikiwa zimerekebishwa kwa wepesi zaidi.