Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia Arusha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hadi sasa Tanzania imetekeleza Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG’s).
Akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya wanawake Dunia ambapo kitaifa yamefanyika mjini Arusha, Rais Dkt Samia amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza umasikini kwa kiwango cha asilimia 26 ikiwa ni lengo la kwanza la Mpango huo unaolenga kupunguza umasikini ilifikapo mwaka 2030.
Ametaja lengo namba mbili ambalo limefanikiwa kwa asilimia mia moja kuwa ni kukomesha njaa na kuongeza kuwa kwa sasa nchi inajitegemea kwa chakula kwa asilimia 128.

“Tunapoadhimisha siku hii tutambue na kuwapongeza wanawake shupavu ambao walipambana katikati ya mfumo dume kufikia hapa, na nchi ipo kwenye hatua mbalimbali za kuchambua sera na sheria ili kulinda haki za mwanamke na mtoto wa kike ambapo pia tupo hatua nzuri ya kutimiza malengo yote ya Malengo ya Maendeleo Endelevu”
“Katika Lengo la nne la afya njema na ustawi, nchi yetu imepiga hatua kwenye eneo la miundombinu kuanzia ngazi ya Zahanati hadi hospitali za rufaa, ununuzi wa vifaa tiba pamoja kukuza ujuzi na utaalamu”
Rais Dkt Samia amesema kutokana na uwekezaji huo vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vimepungua kutoka vifo 1,500 kwa vizazi hai laki moja hadi kufikia vifo 104 kwa vizazi hai laki moja.
Kwa upande wa elimu amesema kwa sasa kuwa usawa wa upatikaji wa elimu kati ya mtoto wa kike na kiume tofauti na hapo awali akitolea mfano usaili wa masomo kwa mwaka huu kuanzia shule za msingi hadi sekondari ambapo kiwango cha watoto wa kike kimepanda na kufikia asilimia 51.

Kuhusu usawa wa kijinsia amesema huko nyuma nafasi za kufanya maamuzi hazikuwa na uwakilishi wa wanawake kama ilivyo sasa ambapo nafasi mbalimbali za kutoa maamuzi kama vile Bunge zimekuwa na uwakilishi wa kuridhirisha.
Kuhusu Nishati amesema Kwa sasa Vijiji vyote nchini vimeunganishwa na nishati safi na sasa hatua inayoendelea ni kuunganisha nishati hiyo kwenye vitongoji.
“Mbali na malengo hayo lakini malengo mengine kama vile maji safi na salama, kazi zenye staha na ukuzaji kiuchumi, viwanda ubunifu na miundombinu, miji na jamii Endelevu pamoja na matumizi na uzalishaji bora navyo tumevifikia”
“Malengo mengine ni kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi, kuendeleza uhali katika jamii, kulinda uhai katika ardhi, amani, haki na Taasisi madhubuti pamoja na ushirikiano ili kufanikisha malengo, yote haya tumeyafikia”

Katika hatua nyingine Rais Dkt Samia ametaka suala la ardhi lipewe kipaumbele Kwani katika kizazi chenye usawa wanawake na wanaume wote wana haki ya kumiliki ardhi.
Aidha amewataka wazazi kuhakikisha suala la maadili linapewa kipaumbele katika malezi ili kujenga kizazi chenye kuheshimiana.
“Tanzania tunakabiliwa na tatizo kubwa la maadili Kwa watoto wetu, katika nafasi mbalimbali nilizoshika serikalini nimejionea mengi, kazi hii ni ya Jamii nzima na siyo kuiachia serikali, tunataka kuwa na kizazi chenye kuheshimiana, wanaume wazungumze agenda za wanawake na wanawake hivyo hivyo”
Awali akimkaribisha Rais, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amesema takribani watu elfu 28 wamepita kwenye mabanda mbalimbali yaliyokuwepo kwa muda wa wiki moja Jijini hapa na kupata elimu, msaada wa kisheria pamoja na huduma mbalimbali.

Akitoa salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amesema Kuna haja ya Wizara ya Katiba na Sheria kufanya kazi kwa kushirikiana na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwani wananchi wengi hawana uwezo wa kuwalipa Wanasheria kwenye migogoro inayowakabili husika masuala ya ardhi.
“Mheshimiwa Rais, TLS wana Wanasheria 882, hawa tukishirikiana nao kwa kuwalipa posho kidogo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wetu” amesema Makonda.