Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inatarajia kunadi vitalu 26 vya gesi asilia na mafuta kwa lengo la kuvutia wawekezaji ili kuchangia maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam Machi 5, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kongamano la 11 na Maonesho ya Petroli nchi Wanachama Afrika Mashariki (EAPCE’25).

Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni akizungumza na vyombo vya habari kuhusu zoezi la Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu nchini Tanzania wakati wa Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaoendelea jijini Dar es Salaam.

Sangweni amesema kuwa kati ya vitalu 26 vitakavyonadiwa, 23 vinapatikana katika Bahari ya Hindi, huku vitatu vikiwa katika Ziwa Tanganyika. Ameeleza kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi katika maeneo hayo, kazi inaendelea ya kuzihakiki.

“Mpango wa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuweka nguvu zaidi katika suala la utafutaji wa mafuta na gesi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inahamasisha nishati safi ya kupikia,” amesema Sangweni.

Amesisitiza kuwa mwaka huu kwao ni muhimu kwani kati ya shughuli wanazofanya ni kunadi na kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya utafutaji wa mafuta na gesi na kwa kuanzia PURA tayari wana maeneo hayo ambayo wameyawekea mipaka ili waweze kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza na kuanza shughuli hizo hapa nchini.

Aidha amesema kama watu wanavyofahamu Tanzania imegundua gesi kiasi cha futi za ujazo Trilioni 57.54 na kwamba gesi iliyogundulika kuna uhakika wa kupata soko hapa nchini na masoko ya nje kama Japan, Korea na nchi nyinginezo.

Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni akifanya wasilisho kwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya petroli kuhusu vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia zinavyonadiwa, wakati wa Mkutano wa 11 wa Petroli ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaoendelea jijini Dar es Salaam.