Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kielelezo cha uwazi na ni muhimu kwa kuwa mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Jaji Mwambegele amesema licha ya umuhimu huo mawakala hao wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura. Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima,” amesema.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesema Tume imetoa kibali kwa asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hizo, taasisi tisa ni za kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi.
Amewasisitiza watendaji hao kutoa ushirikiano kwa taasisi, asasi na waangalizi waliopata vibali watakapofika kwenye maeneo yao kwa kuwa ni wadau muhimu na akaongeza kuwa Tume itawapa vitambulisho kwa urahisi wa kuwatambua.
Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwa kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa na vinatakiwa kutumika katika awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari.
“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu. Aidha, mnapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza,” amesema.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari mkoani Dar es Salaam ambao utaanza tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
