RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron amelihutubia taifa lake kuhusu hali ya sintofahamu iliyopo duniani kutokana na mabadiliko makubwa ya sera ya Marekani juu ya Ukraine katika utawala wa Rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Kwenye hotuba hiyo kwa taifa iliyorushwa moja kwa moja na televisheni, Rais Macron kwa sehemu kubwa ameitumia kuzungumzia hatma ya usalama na ulinzi wa bara la Ulaya na jukumu la viongozi wa bara hilo katika kuisaidia Ukraine.
Macron ameitaja Urusi kuwa “kitisho kwa Ufaransa na Ulaya”, na ametahadharisha kwamba itakuwa kosa kubwa iwapo Ulaya itachagua kuwa “mtizamaji” katika wakati wa sasa aliosema ni “hatari duniani”.
Kiongozi huyo alisema ili kuhakikisha usalama wa Ulaya, analenga kujadili na viongozi wenzake leo Alhamisi mjini Brussels, juu ya uwezekano wa bara hilo kutumia makombora ya nyuklia ya Ufaransa kama mwavuli wa kinga dhidi ya vitisho kutoka Urusi.
Kwa zaidi ya miongo saba mataifa yenye silaha za nyuklia duniani yamekuwa yakizitumia kama ngao ya kuepuka mashambulizi kutoka nchi nyingine. Barani Ulaya ni Ufaransa na Uingereza pekee ndiyo madola yenye silaha zake yenyewe za nyuklia.
Nchi nyingine hasa zilizo wanachama wa Jumuiya ya NATO zimekuwa zikiitegemea Marekani kutoa kinga dhidi ya mashambulizi ya nyuklia kutoka madola hasimu mfano wa Urusi.
Hata hivyo mabadiliko ya sera za Marekani tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump yamesababisha wasiwasi kuwa taifa hilo lenye nguvu linawatupa mkono washirika wake wa Ulaya.
Rais Macron amesema atawaambia viongozi wenzake wa Ulaya kwenye mkutano unaofanyika wa mjini Brussels kwamba wanaweza kuitumainia Ufaransa na silaha zake za nyuklia kutoa kinga kwa bara hilo.
Matamshi yake yanafuatia pendekezo lililotolewa hivi karibu na mwanasiasa anayetazamiwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz la kutumiwa silaha za nyuklia za Ufaransa kama ngao kwa mataifa ya Umoja ya Umoja wa Ulaya.
