Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni kielelezo cha mafanikio makubwa ya serikali katika kuboresha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.

Ameyasema hayo leo Machi 05, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya utoaji elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi nchini na miaka 30 ya VETA.

Amesema kuwa, kwa kipindi cha miongo mitatu, VETA imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwajengea Watanzania uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa, na kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi na imekuwa ni taasisi muhimu inayochangia rasilimali watu yenye ujuzi inayohudumu katika sekta mbalimbali, ikiwemo Viwanda, Kilimo, Ujenzi, Teknolojia, Nishati na huduma na Utalii.

“Mwaka huu tutaadhimisha miaka 30 ya VETA ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge mwaka 1994 na kuanza kazi rasmi mwaka 1995. Kabla ya VETA kulikuwa na Idara ya Mafunzo na Majaribio ya Ufundi Stadi (NVTD) katika Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii ambayo ilianzishwa mwaka 1975.

“Maadhimisho haya ni fursa ya kipekee kwa jamii kusherehekea mchango wa ufundi stadi katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii, huku tukijipanga kuimarisha sekta ya ufundi stadi ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya soko la ajira,” amesema.

Ameeleza kuwa, kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika kuanzia Machi 18 hadi 21 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) na mgeni rasmi ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Ukuzaji Stadi na Ubunifu kwa Maendeleo ya Jamii na Taifa’.

Amesema kuwa, shughuli mbalimbali zitafanyika katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho hayo, ikiwemo kutoa huduma kwa jamii, kuendesha maonesho ya ubunifu wa teknolojia pamoja na kutoa tuzo na vyeti vya heshima kwa watu mbambali kwa mchango wao katika shughuli za maendeleo ya Ufundi Stadi nchini.

“Maadhimisho haya ya miaka 50 ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na miaka 30 ya VETA yanakuja wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kukamilishwa ujenzi wa vyuo vya VETA vya hadhi ya kimkoa, katika mikoa yote ambayo haina vyuo vya VETA na vyuo vya VETA vyenye hadhi ya kiwilaya katika wilaya zote ambazo hazina vyuo hivyo.

“Kwahiyo sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa chuo chenye hadhi ya Mkoa cha VETA kwa Mkoa wa Songwe na tunaendelea na ujenzi wa vyuo 64 katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazina vyuo hivyo,” amesema na kuongeza:

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha katika maadhimisho haya kote nchini yanakoendelea na kipekee katika kilele cha maadhimisho jijini Dar es Salaam ili tukajionee na kujadili umuhimu wa elimu na ujuzi. Kulingana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023,”.