Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry William Silaa , ameshiriki katika Mkutano wa Dunia wa Masuala ya Mawasiliano ya Simu (Mobile World Congress 2025) unaofanyika kuanzia tarehe 3 – 5 Machi 2025 katika mji wa Barcelona, Hispania.

Katika mkutano huo, Waziri Silaa ameshiriki mijadala mbalimbali ikiwemo ujumuishaji wa uunganisho wa moja kwa moja kwa kifaa (Direct to Device – D2D) katika mfumo wa mawasiliano na mbinu za kukabiliana na changamoto za masafa. Aidha, amejadili uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USF) katika nchi za Afrika, ambapo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wa Tanzania (UCSAF) umetajwa kuwa miongoni mwa mifano bora ya uwazi na mafanikio. Mada nyingine iliyojadiliwa ni uwepo wa bei nafuu za masafa zinazochochea usawa wa mawasiliano.

Waziri Silaa ameshiriki pia mjadala wa Kitaifa (National Dialogue: Tanzania Towards a Fully Digitalized Economy) uliofanyika pembezoni mwa mkutano huo kwa kushirikiana na Kampuni ya Watoa Huduma za Mawasiliano Duniani (GSMA), waandaaji wakuu wa MWC 2025.

Katika mjadala huo, GSMA iliwasilisha taarifa ya tathmini ya changamoto zinazokabili sekta ya mawasiliano katika nchi nne za Afrika, ambazo ni Nigeria, Kenya, Ethiopia, Zambia na Afrika Kusini.

Waziri Silaa ametumia mkutano huo kutangaza Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Tanzania, uliozinduliwa tarehe 29 Julai 2024 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akihamasisha GSMA kuwakaribisha wanachama wake kushiriki katika utekelezaji wake.

Mkutano wa Dunia wa Masuala ya Mawasiliano ya Simu wa mwaka 2025 unakutanisha watunga sera wa sekta ya mawasiliano, wabunifu wa mifumo na programu mbalimbali za kiteknolojia, watoa huduma za simu za mkononi, pamoja na watafiti.

MWC 2025 ni jukwaa muhimu kwa makampuni ya teknolojia kuonesha bidhaa mpya, zikiwemo simu za mkononi, vifaa vya mawasiliano, pamoja na suluhisho mbalimbali za kiteknolojia.