Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita kuna matukio mawili makubwa ambayo yametokea na nadhani kwa uzito wake yanipasa niyaandike katika makala hii.

Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya ziara ya kihistoria jijini Tanga. Ameangalia miradi ya maendeleo ya serikali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 600 na miradi ya sekta binafsi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 500. Unakumbuka kuwa Rais Samia alikuwa ziarani Tanga wakati Rais John Pombe Magufuli anafariki dunia Machi 17, 2021?

Sitanii, Rais Samia ametembelea Bandari ya Tanga, akashuhudia maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari ya Tanga na akasema maboresho yaliyofanyika katika bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi yanaifanya Tanzania kuchukua nafasi yake ya kuwa lango la Afrika. Kwa upande mwingine, amezindua miradi mingi, ukiwamo wa GBP waliowekeza katika gesi kwa thamani ya dola milioni 50.

Nakiri kati ya yote, nimefurahishwa na Rais Samia kuzitembelea wilaya zote nane za Tanga. Ziara kama hizi za viongozi wa kitaifa zinaleta maendeleo kwa kasi, kwani hata watendaji wanaona wanamulikwa na serikali na vyombo vya dola. Nafahamu katika ziara hii Rais Samia amezindua miradi mingi ukiwamo mradi wa maji wa Ngombeza, unaozipatia maji wilaya za Handeni, Korogwe na nyingine.

Ni matumiani yangu kuwa Rais Samia ataendelea kufanya ziara za aina hii na kuichangamsha mikoa ambayo inapelekewa fedha nyingi za maendeleo. Miaka ya nyuma Mwalimu Julius Nyerere alikuwa anafanya ziara nyingi za aina hii mikoani. Ziara hizi zilikuwa na manufaa makubwa, hivyo kwa Rais Samia kufanya ziara za aina hii anapata fursa ya kufahamu na kuratibu maendeleo ya taifa kupitia mikoa anayoitembelea.

Suala la pili katika makala hii, Jumapili ya Machi 2, 2025 Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) tulipata fursa ya kukutana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, pamoja na viongozi waandamizi wa chama hicho. Tulikuwa na mjadala na viongozi hao, ambao wameeleza mambo mengi, lakini kimsingi wamejikita kwenye mfumo wa uchaguzi.

Lissu amesema kigezo cha uwakilishi duniani kote ni idadi ya watu, ila kwa Tanzania kigezo kinachofuatwa ni mazingira na ubora wa miundombinu. Kwa maneno yake anasema Jimbo la Temeke, mwaka 2020 mbunge mmoja amechaguliwa na wapigakura 478,000, wakati wabunge 50 wa Zanzibar wanachaguliwa na wapigakura 566,000.

Nimemuuliza Lissu yeye angekuwa na mamlaka Zanzibar angeipa wabunge wangapi? Akasema kigezo kiwe idadi ya watu. Kimsingi katika hili, sikubaliani na Lissu. Tanganyika na Zanzibar ziliungana zikiwa nchi huru mbili. Sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Serikali mbili. Kwa mantiki hiyo, hauwezi kusema Zanzibar iwakilishwe na mbunge mmoja.

Suala jingine, Lissu amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi si huru. Nimerejea vifungu vya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi juu ya utaratibu mpya unaoanzishwa na sheria iliyotungwa mwaka 2024 ambapo sasa makamishna wa tume wanaomba kazi, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, Rais anapelekewa majina matatu – matatu, ili ateue mmoja katika nafasi hizo. Lissu alipoona kibano kimemzidi akaishia kusema sheria iliyotungwa inakinzana na Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977.

Hoja nyingine aliyoisema Lissu ni utaratibu wa wagombea wa upinzani kuenguliwa kwa madai kuwa wanajaza vibaya fomu au hawajui kusoma na kuandika. Binafsi nakubaliana na Lissu katika hoja hii. Si sahihi wagombea kuenguliwa kwa vigezo ambavyo kila mwenye macho anaona ni mchezo mchafu. Tatizo hili lilianza mwaka 2019 na 2020, ambalo limeendelea hadi sasa. Inabidi lisahihishwe.

Hoja nyingine aliyoitoa Lissu ni kuwa uapishaji wa mawakala wa vyama vya siasa ni tatizo. Pia katika hili nakubaliana na Lissu, kwamba imekuwa kawaida sasa wakati wa uchaguzi, mawakala wa vyama vya upinzani kuapishwa inakuwa ni mbinde. Misingi ya utawala bora inataka kila chama kilichosimamisha mgombea kipewe fursa ya kuwa na wakala, ila wanachotendewa wapinzani kwa mawakala kuapishwa usiku au fomu kupotezwa, si sawa.

Lissu amezungumza mambo kadhaa, ila la mwisho ni hili ambalo anasema ‘No Reform, No Election’ (Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi). Nimemuuliza Lissu ikitokea Watanzania wakakataa kushiriki maandamano anayoyategemea kama silaha ya kuzuia uchaguzi atafanya nini? Atajiuzulu uenyekiti wa CHADEMA? Kimsingi japo aliomba radhi baadaye, aliishia kutukana.

Baada ya kumbana zaidi, akasema: “Wakikataa kushiriki maandamano ya kuzuia uchaguzi, basi tutajua kuwa wamechagua mfumo wa sasa wa uchaguzi.” Akasisitiza kuwa yeye kama Mkristo, hawezi kushiriki dhambi ya uchaguzi kutofuata misingi ya sheria. Hoja hii, inawezekana hesabu za Lissu hazijakaa sawa. Nimemweleza kuwa ndani ya CHADEMA, wapo watu wanataka kugombea ubunge na udinwani, hivyo msimamo huu unawakwanza ndani ya chama hicho.

Kwa vyovyote iwavyo, Tanzania ni nchi yetu sote. Dhana ya kutumia vurugu na nguvu kudai haki, nadhani Lissu anataka kuilinganisha Tanzania na Kenya, ila anasahau jambo moja. Tanzania tumekuwa tukifanya uamuzi wa mambo yetu kwa kujenga hoja na si kutumia mabavu.

Hata Uhuru wakati sisi tuliupata kwa mazungumzo, Kenya waliupata kwa vuguvugu la vita la MAUMAU. Kwamba watazuia uchaguzi, sina uhakika kama ni wazo sahihi. Ni heri washiriki mchakato wajenge chama kuliko kususia. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827