Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wanaendelea kutekeleza miradi ya maji yenye thamani ya Sh bilioni 4.5 katika Halmashauri ya Bukoba ambayo itanufaisha vijiji 17 na wananchi 29,000.
Meneja wa Ruwasa Halmashauri ya Bukoba, Evarsta Mgaya amesema kuwa miradi hiyo ni mipya katika mwaka wa fedha 2024/2025 na baadhi imeanza kukamilika hivyo kabla ya mwaka wa fedha haujaisha mwezi Julai miradi hiyo itaanza kutoa maji na kunufaisha wananchi.

Kamati ya siasa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Bukoba Vijijini imefanya ziara ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na kwa mujibu wa meneja huyo amesema kuwa miradi hiyo itakapokamilika wananchi wa Bukoba Vijijini asilimia 83 watakuwa na uwezekano wa kupata maji safi na salama.
“Nyote mtakumbuka kuwa wengi walipata adha kubwa sana kupata maji wakati Ruwasa inaanzishwa hapa wengi hawakuwa na maji ya bomba labda visima vidogo lakini kwa sasa serikali imefanya kazi kubwa sana ya kupeleka maji majumbani, watu wanaoga shughuli za uchumi zinaendelea hii ni hatua sana na Ilani imetekelezwa kwa kiasi kikubwa,”amesema Mgaya.

Amesema kuwa miradi mingine mikubwa inaendelea kusanifiwa huku vijiji vingine ambavyo havijawai kupata maji vikiendelea kuwekwa kwenye mpango ili kutimiza adhima ya serikali ya kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata maji safi na salama kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025 na asilimia 95 kwa wananchi waishio mjini.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Bukoba, Evarsta Babyegea kupitia miradi hiyo amewaomba wakandarasi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili wananchi kupata maji na kuendela na shughuli za uzalishaji.
amesema chama cha mapinduzi katika halmashauri ya bukoba kinaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji kupitia ruwasa kwani hata vijiji ambavyo watumishi walipangiwa kazi na kupakataa kwa ajili ya kutopatikana kwa maji sasa wanapakimbilia kwani hakuna adha hiyo.

Katibu ya siasa na uenezi Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Bukoba Vijijini Diocles Byabato licha ya pongezi nyingi kwa Ruwasa kwa kutekeleza miradi ya maji kwa weledi amewaomba kukamilisha kiporo cha usambazaji maji katika mji mdogo wa kemondo ili kuondoa adha kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao.
Amesema kwa upande wa maji Ilani imetekelezwa vya kutosha na huduma ya maji katika Jimbo la Bukoba lililokubwa na kero kwa miaka ya nyuma sasa ni shangwe na matumaini ni kuwa miaka michache ijayo wananchi wote watafikiwa na maji.
