Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani M. Lwamo amesema kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Ameeleza kuwa makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu na kwamba katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Tume imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 690,763,401,639.06 sawa na aslimia 69.08 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 4 Machi, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, Dodoma na kueleza kuwa kuimarika huko kunatokana na rasilimali madini, kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini.

Aidha amesema Tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini, wasambaza bidhaa na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.
Amesema Katika kipindi rejewa, jumla ya Mipango 1,076 ya Ushirikishwaji wa Tanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,047 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 29 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho.
“Tume imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa Ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Kampuni mbalimbali za uchimbaji ambapo katika kipindi rejewa Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,874 ambapo kati ya hizo 19,371 ni Watanzania sawa na asilimia 97.5 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.5 ya ajira zote zilizozalishwa, “amesema
Ameeleza kuwa jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.
“Katika kuendelea kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini, Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi rejewa, Tume imefanikiwa kutenga maeneo 58 kwa ajili ya Wachimbaji wadogo katika Mikoa mbalimbali,

Tume pia imeendelea kuwatengenezea mazingira rafiki kwa ajili ya kupata leseni za uchimbaji pamoja na kuwaunganisha na Taasisi za kifedha ili wapate mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za uchimbaji ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kijiolojia Tanzania (GST) katika kuyafanyia utafiti maeneo mbalimbali ili kuwawezesha Wachimbaji kupata taarifa sahihi za uwepo wa rasilimali Madini na kufanya uchimbaji wenye tija, “ameeleza
Mhandisi Lwamo pia ametumia nafasi hiyo kuzungumzia maeneo ya kipaumbele kwenye tume hiyo yatakayoleta ufanisi kuwa ni
Kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa Tume ya Madini,kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini pamoja na kuvutia uwekezaji.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa;
Kuendelea kuboresha mazingira yatakayowezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini,kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano kati ya Tume na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini na kuendeleza rasilimali watu na kuboresha ustawi wa watumishi.
“Katika kuleta ufanisi,Tume imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Madini nchini kwa kutoa leseni kubwa kwa Kampuni mbalimbali za uchimbaji ambapo leseni hizo zilitolewa kwa kampuni mbalimbali kuanzia Mwaka 2021 hadi Januari, 2025 ambapo utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika Sekta ya Madini pamoja na Sekta nyingine fungamanishi hapa nchini, “ameeleza.

Pamoja na hayo amesema Tume imeendelea kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa.
” Katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Ukaguzi ulifanyika katika maghala ya kuhifadhia baruti kwenye mikoa 30 ya kimadini, ambapo jumla ya bohari (magazine) 164, Stoo (stores) 268 na masanduku (boxes) 207 yalikaguliwa, “amesema.
Amesema mafunzo kuhusu masuala ya usalama, afya, mazingira pamoja na usimamizi wa baruti yalitolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini katika Mikoa mbalimbali ya kimadini nchini ambapo jumla ya wachimbaji wa Madini 11,478 walishiriki mafunzo hayo.