*Asema CHADEMA walionyesha ubinafsi bila kujali masilahi ya Watanzania wote

*Walitaka wao na CCM pekee washirikiane kuandika Katiba mpya

*Asema ‘No reforms, no election’ ni ndoto na kinyume cha Katiba, sheria za nchi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMwedia, Dar es Salaam

Hatimaye siri ya kuvunjika kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imewekwa hadharani; JAMHURI linaripoti.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema kuna hoja kadhaa zilizopelekwa na CHADEMA ambazo zisingeweza kutekelezeka.

Kwa ujumla, CHADEMA walikwenda kwenye meza ya maridhiano na CCM wakiwa na hoja 11, lakini mazungumzo yalivunjika baada ya hoja tano tu kujadiliwa; nne zilikubaliwa na pande zote mbili, huku moja ikipingwa na CCM.

Hoja iliyopingwa vikali, kwa mujibu wa Wasira, ni ile ya CHADEMA kutaka wao na CCM ndio wakae mezani na kuandika Katiba mpya.

Yafuatayo ni mazungumzo kati ya JAMHURI na Wasira.

JAMHURI: Baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani alifungua milango ya maridhiano. Ni kwa nini mazungumzo ya maridhiano kati ya CCM na CHADEMA yalivunjika?

WASIRA: Katika mariadhiano haya, pande zote mbili zilikuja na hoja nzito nzito. Upande wa CCM uliongozwa na mtu niliyechukua nafasi yake, Abdulrahman Kinana.

CHADEMA walishusha ajenda (hoja) 11, ila walikubaliana wazungume kwanza nusu ya zile ajenda, halafu zilizosalia zitakuja ‘phase’ (awamu) ya pili.

Ajenda ya kwanza ilikuwa ni wale watu waliokuwa wamekimbia nchi wahakikishiwe usalama wao. Hao ni pamoja na Tundu Lissu, Godbless Lema na Ezekiah Wenje.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia vikao halali vya Bunge, akatangaza kuwa wanasiasa hao wanarudi na watakuwa salama kabisa.

Wanasiasa hawa walirudi na wako salama mpaka sasa; ukiondoa ndoto za Lissu ambaye akiota tu, anakimbilia Ubalozi wa Ujerumani. Ingekuwa watu wanakimbia (kwa ndoto tu) mbona marais wote wangekwisha!

Sasa yeye akikimbia, anasindikizwa kwenda nyumbani kwake Ubelgiji. Hii ilikuwa ‘condition’ (hoja) namba moja. Ikatekelezwa.

Hoja ya pili, CHADEMA waliomba vyama vya siasa viruhusiwe kuendesha shughuli za mikutano ya hadhara bila vikwazo.

Januari 4, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan akasema amekubali. Wanaendelea na mikutano yao na mpaka leo wanaendelea vizuri kabisa! Walikuja hapa wakasema wanataka maandamano; wakapewa polisi wawasindikize.

Wakawa wanawasindikiza hata wanaochoka (waandamanaji wanachama wa CHADEMA), askari polisi wanawatoa na kuwapa ‘glucose’ ili wapate nguvu waendelee.

Mikutano wamefanya mingi sana, karibu maeneo yote nchini na hakukuwa na usumbufu wowote, isipokuwa walipoanza kuleta mazingira ya uvunjifu wa amani kule Mbeya, wakazuiwa kidogo; ‘otherwise’ walitembea nchi yote. Hoja namba mbili ikakubaliwa.

Hoja ya tatu. Mwaka 2020 kuna watu wao 400 walikuwa wamekamatwa na kufunguliwa kesi katika mahakama mbalimbali nchini, wengine wako mahabusu na wengine kufungwa. Ili kuleta maridhiano na ‘goodwill’, wakaomba kesi hizo zitazamwe upya.

Waliokuwa wamefungwa waliachiwa kwa huruma ya Rais Samia, kwa sababu ana mamlaka kikatiba. Wengine Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) akapitia kesi zao, wakaachiwa isipokuwa kesi mbili.

Moja ilikuwa Pwani na nyingine Njombe; za mauaji. Ile kesi ya Njombe imehukumiwa juzi (Jumatatu iliyopita) na bahati nzuri wameshinda. Hili ni la tatu.

Hoja ya nne, CHADEMA walitaka wale wabunge wanawake 19 wanachama wao, waliokuwa wanabishana (nao). Wakataka waondolewe bungeni.

Sasa kuondolewa bungeni ikawa ngumu, kwa sababu wale watu walishahukumiwa na chama chao, lakini walikata rufani Mahakama ya Rufaa Tanzania!

Chama chao (CHADEMA) kinawaambia lazima utawala uwe wa sheria. Sasa utawala wa sheria tena Rais aiingilie Mahakama ya Rufani afute kesi iliyopo mahakamani wakati yeye hakuipeleka!

‘Criminal cases’ (kesi za jinai) unaweza kuzifuta kwa sababu Serikali (Jamhuri) ndiyo inashtaki. Hii ni watu binafsi wanashtaki chama chao, sasa Rais anaingiaje hapo na kwa mamlaka yapi? Hilo likashindikana. Wakasema kushindikana kwa hilo kunawapa matatizo.

Hoja ya tano walitaka CCM ishirikiane nao (CHADEMA) kuandika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waliwasilisha mapendekezo ya Katiba mpya wanataka iweje, CCM tukasema haiwezekani. Hii Katiba mpya si ya vyama, ni ya Watanzania wote, kwa hiyo CCM haiwezi kushirikiana na chama kimoja tu ‘ku-draft’ Katiba.

Liliposhindikana hilo, wakasema sasa mazungumzo hayapo, wakasitisha mazungumzo… wao ndio waliositisha mazungumzo, hata zile hoja zilizosalia hawakuzileta tena.

JAMHURI: Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, hoja sita zilizosalia ni zipi? Je, unaweza kuziweka hadharani ili wananchi wazifahamu?

WASIRA: Mimi ninazijua, lakini sitaki kuwasemea. Nendeni mkawaulize zile hoja nyingine wamezipeleka wapi?

Kwa hiyo utaona hoja kubwa zilikuwa ni hizo (tano za mwanzo). Ninasema na wakibisha nitaleta muhtasari wa kikao. Tulikataa (kukaa na kuandika Katiba mpya).

Sisi hatuwezi kula njama na chama kimoja cha siasa kuandika Katiba ya Jamhuri ya Muungano! Lazima tuwe na utaratibu.

Hata hivyo, ni wazi walikuwa wanatikisa kiberiti wakakuta kimejaa. Sasa hapo ndipo ‘problems’ (matatizo) zilipoanzia.

Wakati wao wanafika hapa, mwenzao (Rais Samia) alikuwa ameunda Kikosi Kazi, na chenyewe kinashauri mambo ambayo yanafanana na hayo, hasa lile la kuruhusu vyama kufanya mikutano na maandamano [wakagoma kushiriki].

JAMHURI: Kuna marekebisho kadhaa ya sheria yamefanywa kukidhi matakwa ya wananchi, je, CHADEMA walishirikishwa katika haya?

Ndiyo! Baada ya kuona muda uliopo ni mfupi, hautoshi kuandika Katiba mpya (kabla ya Uchaguzi Mkuu), walisema tutazame kitu kinaitwa ‘reforms’ na zitazamwe sheria tatu; Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kwamba sheria hizi zifanyiwe marekebisho ili kabla ya kwenda kwenye hoja ya Katiba mpya baada ya uchaguzi, basi kwanza uchaguzi ufanyike kutokana na marekebisho hayo.

Sasa tumefanya ‘reforms’, miswada ikapelekwa bungeni, lakini kamati husika (Kamati ya Kudumu ya Bunge) ikasema wale wote ambao wanapenda kwenda kutoa maoni, wakatoe!

Walikwenda. Hata wao (CHADEMA) walikwenda! Hii haina ubishi maana rekodi za Bunge (Hansard) zipo. Hata kwenye kamati kuna Hansard, hivyo hauwezi kubisha kuwa haukwenda!

Mnyika (John Mnyika, Katibu Mkuu wa CHADEMA) alikwenda, BAWACHA (Baraza la Wanawake CHADEMA) na BAVICHA (Baraza la Vijana CHADEMA) walikwenda kutoa maoni.

Na taasisi nyingi mno zilikwenda. Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) walikwenda; CCT walikwenda; Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) walikwenda na hata wale wanaopingana na Bakwata walikwenda. Taasisi zisizokuwa za kiserikali nazo zilikwenda.

Inakadiriwa kuwa watu 3,900 walifika na kutoa maoni na maoni yao yalisikilizwa vizuri. Kwa mfano maoni yalitolewa kusiwepo mbunge wa kupita bila kupingwa; kwamba jimboni ukikosa mpinzani wa chama kingine unatangazwa kuwa umeshinda.

Kwa sheria hii mpya, hauwezi kutangazwa kuwa mshindi, lazima upigiwe kura za ndiyo au hapana. Mabadiliko haya yalitokana na maoni yao.

JAMHURI: Baada ya uchaguzi wa ndani ya chama, CHADEMA wamekuja na kaulimbiu ya ‘No reforms, no election’; kwamba hakutakuwa na uchaguzi (mkuu) bila kuwapo mabadiliko. Hili CCM mnalisemaje?

WASIRA: Na sisi tunauliza ‘reforms’ zipi? Maana ‘tulikwisha-reform’! Lakini kwa hulka yao kama walikwenda pale (Kamati ya Bunge) wakatoa maoni na mengine hayakukubaliwa; basi kwao ‘reforms’ haijakubalika. Yaani wao wanataka kila kitu wanachotaka, kiwe. Nchi haiendeshwi namna hiyo.

Kaulimbili ya CHADEMA (No reforms, no election) haina mashiko. Ni propaganda tu.

Kwanza, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, hakuna mtu aliyepewa mamlaka ya kuahirisha uchaguzi. Sasa bila kuwa na mamlaka, lazima utuambie mamlaka yako unayatoa wapi?

Ibara ya 8(1)(a) inasema wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.

Serikali ambayo iko madarakani haina mamlaka ya kuahirisha uchaguzi, Katiba hii haikutoa mamlaka kwa mtu yeyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusema uchaguzi unaahirishwa.

Sasa mtu anaposema uchaguzi uahirishwe; anasema kwa mamlaka yapi? Wewe unasema hivyo kwa mamlaka yapi?

Hakuna mamlaka yoyote ambayo yametolewa na Katiba hii kuhusu mtu au chombo chochote kwamba kinaweza kusema uchaguzi huu haufanyiki. Hakuna!

Wenzetu wanasema wanataka usifanyike, tunawauliza kwa mujibu wa mamlaka yapi? Hakuna mamlaka ya kikatiba wala kisheria ambayo yanampa mtu au taasisi yoyote kusema itazuia uchaguzi.

Itaendelea…