Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amewashauri wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria kutoa maelezo sahihi ili kuwasaidia watoa huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid kutatua changamoto zilizoshindikana na kupata ufumbuzi.
Sagini ametoa ushauri huo leo Machi 01 jijini Arusha wakati alipotembela mabanda ya maonesho katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika kitaifa Machi 8 jijini humo huku ikitanguliwa na maonyesho mbalimbali kutoka taasisi na mashirika.
Aidha migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa ni miongoni mwa changamoto zinazoongoza katika kampeni zinazoendelea kufanywa nchi nzima na wananchi kusisitizwa kuandika wosia ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kutokea katika familia husika.

Sagini amesema kampeni hiyo imelenga kusaidia wananchi wenye shida mbalimbali hivyo ni vema wananchi wenye migogoro kutoa maelezo sahihi kwa wataalam wanaotoa msaada wa kisheria katika kampeni hiyo yatakayosaidia kutatua migogoro yao.
“Hapa wataalam mbalimbali wataongoza kampeni hii kwa ajili ya kusaidia kutatua kero mbalimbali zinazowasibu lakini naomba wananchi muwe na tabia ya kuandika wosia ili kuondoa sintofahamu wakati wa kugawana mali lakini pia kesi za madai za idara mbalimbali ikiwemo idara ya kazi zinazotolewa maamuzi zitatuliwe mapema ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi wanaohitaji haki zao,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mkoa Arusha, Paul Makonda amesema kupitia kampeni hiyo hakuna mwananchi atakayeachwa kupatiwa msaada wa kisheria na kuwasihi watoa huduma za msaada wa kisheria kuwasikiliza vema wananchi ili kutatua changamoto zao.

Wakati huo huo, Mratibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Mkoa wa Arusha, Philemon Mkwai amesema wakala hao kupitia huduma za kidigitali eRITA wanatoa vibali mbalimbali vya vizazi, vifo, ndoa, talaka na udhamini.
Amesema kwa sasa huduma ya usajili ya vizazi inapatikana kwa njia ya kidigitali kupitia tovuti ya RITA, www.rita.go.tz ambapo faida zake ni kupunguza msongamano wa wananchi kupata huduma badala ya kupanga foleni ofisini hivyo watakwenda kuchukua cheti pekee.
