Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ikiwa ni siku chache tu tangu ilipotimia miaka 58 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Hispainia. Historia inatueleza kuwa mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi mbili za Tanzania na Uhispania yaliasisiwa rasmi mnamo februari 23 mwaka 1967. Hivyo basi kupitia mahusiano hayo baina ya nchi hizi mbili yamepelekea kujengeka kwa urafiki mkubwa wa kinchi ambao umekuwa wenye kuzinufaisha nchi zote mbili.

Kwa miongo takribani mitano mpaka kufikia sasa uhusiano huo unatajwa kama uhusiano wenye tija kupitia mashirikiano ya serikali zote mbili katika kuchochea mabadiliko katika nchi zote mbili. Ripoti hii itaangazia baadhi ya hatua muhimu ambazo zimepigwa baina ya serikali za nchi hizi mbili katika kuleta ukuaji wa kimaendeleo ya jumla nchini. Ni dhahiri ya kuwa uhusiano huo umekuwa ukichochea maendeleo katika baadhi ya sekta nchini kama sekta ya nishati,utalii, biashara pamoja na suala zima la miundombinu.

Kupitia mahojiano maalumu ambayo nimefanya na balozi wa Uhispania nchini Tanzania, Jorge Moragas ametoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na mahusiano ya nchi hizi mbili huku akienda mbali zaidi kwa kujibu baadhi ya maswali ambayo aliulizwa kuhusiana na ushirikiano uliokuwepo,uliopo na utakaoendelea kuwepo katika baadhi ya sekta hapa nchini.

Awali akianza kutoa ufafanuzi kuhusu mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Uhispania, Balozi huyo wa Uhispania hapa nchini ambapo ameyaelezea kama mahusiano yenye tija na yenye kujenga kwa kadri siku zinavyozidi kwenda ukilinganisha na miaka ya nyuma uhusiano huo ulipoasisiwa huku akibainisha kuwa uhusiano huo umezidi kuimarika mpaka kufikia hivi karibuni.

UHUSIANO KATIKA SEKTA YA NISHATI

Zikiwa ni wiki chache tu zimepita tangu Tanzania ilipokuwa nchi mwenyeji katika mkutano wa wakuu wa nchi nishati(MISSION 300) uliofanyika mwishoni mwa mwezi januari mwaka huu jijini Dar es salaam na kupitisha azimio la Dar es salaam lililolenga kusaidia upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi millioni 300 barani Afrika mpaka kufikia mwaka 2030. Licha ya mkutano huo kufanyika kwa mafanikio makubwa hapa nchini deni limebaki kwa wahusika kuandaa mikakati thabiti kuona ni kwa jinsi gani mpango huo unakamilika kwa wakati. Changamoto katika suala zima la nishati limekuwa likitiliwa mkazo na serikali ya Tanzania chini ya rais Samia licha ya jitihada zinazofanywa na serikali katika kupunguza changamoto zinazoikabili sekta ya nishati.

Katika kupambana na hilo mwishoni mwa juma liliopita kupitia msemaji mkuu wa serikali Gerson Msigwa alielezea juu ya mwenendo wa mradi mkubwa wa serikali katika bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ukarabati wake uko katika hatua za mwisho kukamilika .Mradi huo unatajwa kama miongoni mwa miradi mikubwa itakayokuja kuleta unafuu katika uzalishaji wa umeme nchini.

Katika mahojiano na balozi huyo wa Uhispania nchini nilipomuuliza swali la kuwa ,Ni kwa jinsi gani serikali ya Hispania itaweza kushirikiana na Tanzania katika kupunguza changamoto katika sekta ya nishati nchini .

Kwa mujibu wake balozi huyo alijibu swali hilo kwa kusema kuwa wanatambua za sekta ya nishati nchini Tanzania huku akitoa pongezi kwa serikali chini rais Samia na waziri wa nishati kwa jitihada za makusudi wanazoendelea kuzifanya kuhakikisha wanaleta maendeleo katika sekta hiyo.

Akiongeza kujibu kuhusu mipango ya uhispania kushirikiana na Tanzania kutatua changamoto katika nishati balozi amesema kuwa katika jitihada za kuunga mkono serikali ya Tanzania kukabliana na changamoto hiyo tayari uhispania imechukua jitihada za makusudi kusaidia utatuzi wa changamoto hiyo kwa kupitia uwekezaji wa makampuni ya uzalishaji nishati ambayo baadhi yake tayari yameshaanza kuwekeza nchini ambapo pia uhispania inashirikiana na umoja wa ulaya katika kupunguza changamoto zinazoikabili sekta hiyo hapa nchini.

”Tunatambua juu ya changamoto za sekta ya nishati nchini Tanzania. Serikali na wizara ya nishati inafanya jitihada kubwa kuboresha sekta hiyo na kwetu sisi tayari tumeanza kuchukua hatua za kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika nishati. Tumechukua hatua kupitia makampuni ya uzalishaji nishati kutoka uhispania kuja kuwekeza nchini na baadhi ya kampuni hizo tayari zimeshaanza utekelezaji wake. Lakini pia tunashirikiana kwa karibu na Umoja wa Ulaya kutoa miradi itakayosaidia kutatua changamoto za niashati.” Alisema.

                               SEKTA YA UTALII.

Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta chache ambazo zinakuwa kwa kasi nchini Tanzania. Ni miezi kadhaa tu imepita tangu nchi ya Tanzania ishinde tuzo kubwa zaidi ya kimataifa ya utalii(World Travel Awards) ambazo zimeitambua Tanzania kuwa sehemu bora zaidi kwa utalii wa safari duniani.

Mafanikio hayo ni wazi kuwa yamekuja kufuatia jitihada za makusudi za rais Samia katika kuongeza ushawishi katika suala zima la utalii wa ndani. Kupitia filamu za kitalii alizoshiriki rais Samia , ROYAL TOUR na AMAZING TANZANIA zimekuwa ni miongoni mwa hatua muhimu katika kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini. Uhispania imekuwa na ushirikiano wa zaidi ya miaka 16 na sekta ya utalii nchini ambapo ushirikiano huo umepelekea Tanzania kupokea idadi ya watalii wengi kutoka nchini Hispania.

Akielezea mahusiano hayo kati ya Uhispania na sekta ya utalii nchini , Balozi Moragas amesema kuwa sekta ya utalii ni sekta ambayo wanashirikiana maslahi na Tanzania huku akikiri kwamba Tanzania ni sehemu inayovutia zaidi kwa utalii kupitia vivutio vyake kama mbuga za wanyama, fukwe na hata majengo ya kihistoria kwa ajili ya kujifunza. Akiongeza balozi huyo pia amesema kuwa Tanzania inapaswa kuitazama Uhispania kama kioo katika kukuza sekta yake ya utalii ambapo ametoa takwimu za kuwa takribani watalii elfu 30 kutoka hispania huja kutalii Tanzania kila mwaka.

Mbali na hayo Balozi huyo alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa ubalozi wa Uhispania unafanya kazi kwa karibu na wizara ya maliasili na utalii chini ya waziri Pindi Chana na iko tayari kugawana uzoefu na Tanzania ,na tayari wameshachukua hatua kwani kampuni kubwa za kitalii zimewekeza nchini na mahusiano yake ni mazuri mpaka sasa.

Aidha pia akiongezea kuhusu suala hili la utalii balozi Moragas amegusia kuhusu eneo la kihistoria la Odvai george linalopatikana katika mkoa wa Arusha hapa nchini ambalo ni kati ya yale maeneo muhimu zaidi duniani. Eneo hilo ambalo linatajwa kama sehemu ambayo viumbe wa kale waliokaribiana na mwili wa mwanadamu waliishi tangu miaka milioni 2 iliyopita. Kwa muda sasa eneo hilo limekuwa likipokea wasomi mbalimbali wa sayansi kutoka sehemu mbalimbali zikiwemo taasisi za elimu kutoka hispania kila mwaka kuja kufanya tafiti mbalimbali za kihistoria katika eneo hilo ambapo balozi huyo amelitaja jambo hilo kama miongoni mwa muhimu na kubainisha kuwa ushirikiano huo ni wa kudumu kati ya uhispania na Tanzania.


BIASHARA NA UWEKEZAJI


Tukigeukia upande huu wa sekta ya biashara na uwekezaji ,ni ukweli ulio wazi ya kwamba sekta hii imekuwa na mchango mkubwa katika suala zima la ukuaji wa uchumi wa nchi. Hapo awali ni dhahiri kuwa hakukuwa na uhusiano imara katika sekta hii baina ya nchi hizi mbili. Serikali ya Tanzania chini ya rais Samia ikiwa bado inazidi kutengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa kigeni kuwekeza nchini muitikio umekuwa ni wenye faida kwani kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la kampuni za kigeni kufanya uwekezaji nchini.

Akitolea maelezo sekta hii Balozi Moragas alikiri kuwa muitikio haukuwa mkubwa kwa wawekezaji kutoka uhispania kuja kuwekeza nchini licha ya baadhi yao kuwepo nchini. Akifafanua zaidi kuhusu hilo balozi huyo amebainisha kuwa tayari wameshachukuwa hatua za awali kuimarisha uhusiano katika sekta ya biashara na serikali ya Tanzania kwa kufungua ofisi za biashara na uchumi(Trade and Economy Office) nchini Tanzania kwa mara ya kwanza.

Akielezea zaidi kituo hicho balozi huyo amesema kuwa kituo hicho kilichofunguliwa na serikali ya uhispania ni sehemu ya uaminifu wao kwa serikali ya Tanzania ambacho pia kimelenga kuleta ushawishi wa makampuni ya kihispania kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini. Aidha pia balozi huyo ameongeza kuwa serikali ya uhispainia iko tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika upande wa miundombinu.

”Serikali ya Uhispania imefungua ofisi ya biashara nchini Tanzania. Ofisi hii imefunguliwa kwa mara ya kwanza hapa na hii ni sehemu ya uaminifu wetu kwa serikali ya Tanzania. Tumekusudia ofisi hii kusimamia na kuziongoza kampuni uwekezaji na wawekezaji kutoka uhispania kuwekeza nchini Tanzania kama sehemu ya kukuza mahusiano kibiashara kati yetu na Tanzania.”

Tukisalia katika upande huo wa miundombinu balozi huyo amedokeza kwa uchache kuwa wako katika hatua nzuri kuingia makubaliano na benki ya dunia kusaidia ukarabati wa daraja la mto msimbazi ambapo amesema kuwa uhispania inataraji kuchangia takribani euro millioni 30 katika mradi huo japo balozi huyo hakutaka kutolea ufafanuzi zaidi jambo hilo kwa liko katika mikono salama ya wizara ya fedha.

MICHEZO

Mbali na hayo aliyoeleza kuhusu sekta hizo balozi huyo alitoa mawazo yake na kupendekeza kuwa angetamani kuona ushirikiano wa mashirikisho ya michezo ya kitanzania na hispania yakishirikiana kwa pamoja katika kuibua vipaji vya michezo . Kupitia hili balozi huyo alikubali pale nilipomuomba kulisimamia jambo hilo na kuahidi kuwa atajiathidi kwa nafasi yake kuweza kulifanikisha hilo.

Katika kuhitimisha makala hii ni dhahiri ya kwamba uhusiano kati ya uhispania na Tanzania umekuwa ni wenye tija lakini mengi zaidi yanahitajika kufanywa na serikali za nchi zote mbili kuhakikisha kuwa uhusiano huo unadumishwa kwa miaka mingi ijayo.