Papa Francis ambaye amelazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki mbili kwa ugonjwa wa maambukizi ya mapafu amewashukuru leo waumini wa kanisa katoliki kote duniani kwa msaada na kumuonesha upendo.

Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ambaye amelazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki mbili kwa ugonjwa wa maambukizi ya mapafu amewashukuru leo waumini wa kanisa katoliki kote duniani kwa msaada na kumuonesha upendo katika kipindi hiki ambacho kimemuweka nje ya kanisa.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 88 ambaye amekuwa akitibiwa katika hospitali ya Gemelli huko Roma tangu Februari 14, alikosa maombi ya jadi ya kila wiki, ambayo badala yake yalichapishwa kwa njia ya barua ambayo Vatican iliitoa mchana wa leo.

Kupitia maombi hayo, Papa amemalizia kwa kutoa wito wa kupatikana kwa amani na kushughulikiwa kwa mizozo inayoendelea duniani ikiwemo huko Ukraine, Gaza, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa sasa hali ya kiongozi huyo bado inafuatiliwa kwa uangalifu mkubwa.