Viongozi wa Ulaya wametangaza kuiunga mkono Ukraine katika mkutano wa kilele uliofanyika London. Wameahidi kutumia fedha zaidi kwenye usalama na kuunda muungano wa kuyalinda makubaliano yoyote ya amani nchini Ukraine.

Mazungumzo hayo, ambayo yaliwaleta Pamoja washirika 18, yalijiri siku mbili tu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumshambulia Volodymyr Zelensky wa Ukraine mbele ya waandishi Habari katika Ikulu ya White House.

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema Uingereza, Ufaransa na “wengine” watashirikiana na Ukraine kuhusu mpango wa kusitisha mapigano, ambao kisha watauwasilisha kwa Washington.

Malumbano ya Trump na Zelensky pia yalizusha maswali mapya kuhusu dhamira ya Marekani kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Starmer alisema Ulaya imejikuta “kwenye njia panda katika historia. Huu sio wakati wa mazungumzo zaidi – ni wakati wa kuchukua hatua.

Ni wakati wa kujitokeza na kuongoza na kuunga mkono mpango mpya wa amani ya haki na ya kudumu.” Bila hakikisho la kuhusika kwa Marekani, “Ulaya lazima ifanye kazi kubwa,” amesema Starmer.