Na Magrethy Katengu,JamhuriMedia, Dar es Salaam
LICHA ya kufanya harambee kwa ajili ya kujenga ofisi ya wafanyabiashara wa Pugu Mnadani imeelezwa kuwa kuna changamoto ya wafanyabiashara kupeleka ngo’mbe zao moja moja kwa moja kwenye machinjio bila kupitisha kwenye Mnada hali inayochangia kurudisha nyuma maendeleo ya mnada mkuu wa Pugu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya harambee hiyo, jijini Dar es Salaam, Diwani wa Kata ya Pugu Stesheni Shaban Mussa amesema kwa sasa mzunguko wa fedha umeshuka katika Mnada huo kutoka shill Bill 1.2 kwa siku hadi kufikia shill mill 800.

Amesema kuwa, kuna wafanyabiashara ambao sio waamini wanabeba mifugo kutoka mikoa mbalimbali hawaifikishi Mnadani na kupeka machinjioni moja kwa moja ambapo kisheria mifugo yote inatakiwa kufika mnadani hapo washushe ili wanunuzi wanunue na kwenda kuchinjwa machinjioni.
“Wanapopeleka ngo’mbe moja kwa moja machinjioni sisi hapa hatuwezi kupata fedha kwani sheria za machinjio haziruhusu kukusanya ushuru ngo’mbe zikiwa nzima, bali ni mifugo iliyochiniwa tu”amesema.
Ameongeza kuwa, wameweka mikakati na mkuu wa minada pamoja na kuzungumza na viongozi wenzake kuhakikisha ngo’mbe zote zinazofika machinjio lazima ziwe na vibali ambayo vimesaini kutoka Mnada mkuu wa Pugu.

Aidha, amesema watakaa na wafanyabiashara kuwaeleza umuhimu wa kulipa kodi kwani changamoto zilizopo Mnadani hapo haziwezi kutatulika kama wao hawalipi kodi na maendeleo hayawezi kupatikana.
“Hapa tumesikiliza changamoto zao wanataka maji, barabara, taa lakini haya yote hayawezi kufanyika bila wao kulipa kodi, mapato yakikusanywa lazima maendeleo yaonekane”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Pugu Mnadani Edward Ntemi amesema kuwa, kulichomsukuma kuanzisha harambee za ujenzi wa ofisi ya wafanyabiashara wa Pugu Mnadani na kushirikisha wadau ni changamoto za wafanyabiashara, ikiwemo kukosa sehemu maalum ya kukutana na kutatua changamoto zao kwa faraghaa.


