Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Mwanza

Mkutano maalumu wa marekebisho ya katiba ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) umefanyika jijini Mwanza kwa kuhusisha wadau mbalimbali wa michezo na viongozi wa Riadha kutoka mikoa zaidi ya 20 ya Tanzania Bara.

Lengo kuu la mkutano huo ni kujadili na kufanya maboresho ya katiba na kanuni zinazohusiana na usimamizi wa mchezo wa riadha nchini.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania Silas Isangi, amesema kuwa maboresho yaliyofanywa katika katiba ya RT ya mwaka 2020 yalikuwa muhimu na yanajumuisha masuala ya elimu, umri wa viongozi, muda wa kukaa madarakani, na vigezo vya kupiga kura kwa wajumbe kutoka mikoa.

Isangi alisema, “Mpiga kura kutoka mkoa atakuwa ni mwenyekiti, na ibara zote zilizokuwa hazijakaa sawa zimeboreshwa.”

Aidha, Rais Isangi alieleza kuwa katiba mpya imepitishwa kwa umoja na kwamba imeridhiwa na kila mjumbe.

“Katiba imepita vizuri, wataifurahia wadau wa michezo, na itakuwa nzuri,” alisema.

Akizungumzia uhaba wa viwanja vya michezo, Isangi amesema kuwa serikali inaendelea kujikita katika ujenzi wa viwanja vya riadha vitakavyosaidia kukuza mchezo huo.

Aliongeza kuwa mikoa ambayo bado haina viwanja bora itatumia viwanja vilivyopo kuendeleza michezo ya riadha, huku akisisitiza kuwa wanariadha wanahitaji miundombinu bora ili kuwakilisha Tanzania kimataifa.

Rais Isangi ametoa rai kwa wenyeviti wa mikoa kuendelea kushirikiana na wanariadha ili kuboresha michezo hiyo baada ya maboresho ya katiba, viongozi.

Akizungumza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Zanzibar, Muhidin Kasunzu, amempogeza Rais wa RT kutokana na mabadiliko hayo kwani kufuatia mabadiliko hayo yatakwenda kuleta chachu ya mchezo huo kwani imetoa nafasi kwa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika mashindano hayo, hivyo matumaini yao ni kuufikisha mchezo huo kimataifa.

Kasunzu ameeleza matarajio yake Mara baada ya maboresho hayo ni wazi kwamba imekuja kurahisisha utendaji kazi kwa viongozi wa RT, kwani hadi kufikia hitimisho hilo ni matakwa ya wadau wa mchezo wa riadha ambao walianza mchakato huo tangu zamani kwa kuhitaji marekebisho ambayo wanaamini kwamba yataleta manufaa makubwa kwao viongozi na wadau wote wa riadha.

Christina Paga Mjumbe kutoka Simiyu, amesema kuwa maboresho ya katiba yamewapa nguvu wajumbe wanawake ambao kimsingi wamepiga hatua katika kutambua nafasi ya mwanamke kwenye Shirikisho hilo.

Hivyo ni muhimu kwao kama wanawake kupata fursa ya uongozi huku akitoa rai kwa wanawake kuwa na mwamko wa kuwania uongozi kwani katiba inatoa nafasi kwao kuweza kuongoza nyadhifa mbalimbali.

Mchakato wa maboresho ya katiba ya RT ulianza miaka kadhaa iliyopita na hatimaye umetamatika Februari 28, 2025, ambapo ulianza kwa kamati ya katiba kuzinduliwa Dar es Salaam tayari kwa kupokea maoni kutoka kwa wadau.

Kamati huru iliundwa na RT kutokana na matakwa ya mkutano mkuu baada ya wanachama wake kutaka maboresho katika baadhi ya vifungu ambavyo waliona vinamapungufu.

Kutokana na uamuzi wa mkutano huo, kamati ya utendaji chini ya Rais wa RT, Silas Isangi, iliazimia kuunda kamati hiyo huru itakayoiandaa rasimu ya mabadiliko ya Katiba, ambayo kimsingi ililenga kufanya maboresho kwa maslahi mapana ya mchezo wa v na sio maslahi binafsi.

Safari yake imehitimishwa jijini Mwanza huku wajumbe kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wameridhia kwa umoja wao na kupitisha maboresho hayo rasmi.