Kibali kilichoiruhusu kampuni kubwa ya mafuta ya Chevron Corp. kusafirisha mafuta ya Venezuela nchini Marekani kitasimamishwa wiki hii, hatua inayoukata uwezo wa kifedha wa taifa hilo la Amerika Kusini.
Akitangaza uamuzi huo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social siku ya Jumatano (Februari 26), Rais Donald Trump ameituhumu serikali ya Rais Nicolas Maduro kwa kile alichosema ni kutokidhi vigezo vya kidemokrasia kwenye uchaguzi wa mwezi Julai na pia kutokuchukuwa hatua za haraka kuwachukuwa wahamiaji wa Venezuela waliopangiwa kufukuzwa Marekani.
Kibali hicho kilitolewa na utawala wa Rais Joe Biden mwaka 2022 baada ya Maduro kukubali kushirikiana na upinzani kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia.
Trump amesema serikali yake inaufuta uamuzi huo mara moja, ambao upinzani unasema uliiwezesha serikali ya Maduro kupata zaidi ya dola bilioni nne.
