Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu kunyongwa hadi kufa mfanyabiashara Khamis Luwonga baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe Naomi Marijani na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.

Hukumu hiyo imetolewa leo Februari 26,2025 na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Mwanga amesema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba mshtakiwa alimuua mkewe na alifanya hivyo kwa makusudi.

“Baada ya kuangalia vielelezo vinaunga mkono stori nzima ya namna tukio la mauaji lilivyotokea. Baada ya tukio kutendeka mshtakiwa alimkunja marehemu kwenye shuka mbili kisha akaupeleka mwili kwenye banda la kuku alikokuwa amechimba shimo.

“Akamkalisha kisha akachukua gunia mbili za mkaa na kumchoma na akahakikisha kila kitu kinateketea halafu mabaki akayapeleka na kwenda kuyafukia shambani kwake.

“Kitendo hiki si cha kibinadamu, kinanifanya niseme alifanya kwa kudhamiria huyu mtu ateketee kabisa…tukio lilifanyika akiwa na akili timamu,” amesema Jaji Mwanga.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava, umeiomba mahakama mabaki ya mwili wa Naomi yakabidhiwe kwa ndugu zake ili wafanye mazishi kwa kuwa hakupewa haki ya maziko.

Wakili anayemtetea mfanyabiashara huyo, Precious Hassan, amesema wanakusudia kukata rufaa kutafuta haki zaidi katika mahakama za juu.

Naye baba mdogo wa marehemu, Robert Marijani, amesema wameridhika na hukumu iliyotolewa na mahakama na wanasubiri mabaki ya mwili wa mtoto wao ili wafanye maziko.

Luwonga alipandishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Julai 30,2019 kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 38, akishtakiwa kwa kosa moja la mauaji ya mkewe Naomi eneo la Gezaulole, Kigamboni.

Ilidaiwa kuwa Julai 16,2019 katika kituo cha Polisi cha Kati wakati Khamisi akiwa anaendelea na harakati za kutoa taarifa Polisi juu ya maendeleo ya mke wake alihojiwa kuhusu jumbe alizodaiwa kutumiwa na mke wake kwani kwa uchunguzi wa kielektroniki ilionyesha kuwa jumbe hizo zilitumwa katika sehemu moja.

Aidha, Jaji alisema ni jukumu la upande wa mashitaka kuthibitisha hatia ya mshitakiwa na katika mauaji inatakiwa kuthibitishwa kama mtu kweli amekufa na kifo chake kuwa sio cha kawaida.

Alisema katika kesi kuna mazingira tofauti kidogo na mazingira yake yanaonyesha kuwa hakukuwa na mwili kuthibitisha kuwa kweli Naomi amekufa na kama hakuna mwili basi uchunguzi wa kitabibu haukufanyika kubaini marehemu alikufa kwa sababu au kutokana na nini.

Aliongeza kuwa kutokana na kesi zilizothibitishwa kutoka nchini India  zilionyedha kuwa kufo cha mtu kinaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa mazingira ambayo kifo hicho kimetokea na uchunguzi unaweza kufanya pasipokuwa na mwili.

“Sio lazima kuwe na mwili ikiwa ni suala la lazima kuwepo na mwili ili kuthibitisha hatia tutawapa na watu upenyo wa kuteketeza ili kukimbia ushahidi,” alisema Jaji Mwanga.

Pia alisema kuwa katika mashahidi hao wapo waliokwenda Morogoro na kwa upande wa mkemia alileta majibu kuwa alishindwa majibu ya moja kwa moja kwani ilibainika mabaki yaliyopatikana yalikuwa ni ya mwanamke lakini haikuthibitishwa kuwa ni ya Naomi .

Jaji Mwanga alisema kuwa katika maelezo ya onyo ya Hamisi alidai kuwa mabaki yale ni ya ya Naomi na alidaiwa kuwa Naomi amefariki na mshitakiwa ndiyo aliyemuua na pia chumba alichokuwa akilala Naomi kilikutwa na mabaki ya damu na yalidaiwa kuwa ni ya Naomi.

Pia kwa mujibu wa maelezo ya onyo ya mshitakiwa alidai kuwa Mei 14,2019 ni siku ambayo hakulala nyumbani kwake kwani alilala kwa Margreth alirudi kwake asubuhi na kumkuta mke wake akimuandaa mtoto kwenda shule alidai alimpita bila kusema chochote na mtoto alichukuliwa na bodaboda kupelekwa shule.

Aliendelea kudai kuwa simu iliita kwa jina la Magreth ndipo Naomi alianza Kumtukana na Hamisi akamwambia achukue chochote anachokitaka kwani hakukuwa na ndoa tena kati yao wakati wa ugomvi Naomi alidondoka chini na kujigonga kichwani na damu zikaanza kutoka akawa analalamika akitetemeka sitomsamehe.

Baadaye alianza kukoroma hadi umauti ulipomfika baada ya Naomi kufa Hamisi akataka kuundoa mwili ndipo alipouzungusha kwenye shuka mbili na baada ya kuona kuwa akitoka na mwili ule kwenye gari akiwa barabarani askari wangemsimamisha na kuuona ndipo alipokumbuka katika banda la kuku kulikuwa na shimo kwa ajili ya kupitisha maji.

Alipokumbuka hili alichukua mwili na kwenda kuuchoma na magunia mawili ya mkaa ili uungue taratibu kwani alihofia kuchoma na kuni zingekuwa nyingi na wakati mwili ulipoungua na kubaki mkaa alimtuma bodaboda kwenda kununua mafuta na alipofiki alikwenda kuyachukulia getini ili asiingie ndani.

Pia jaji aliendelea kusema kuwa maelezo hayo yanaeleza kuwa kwakuwa mafuta ya taa yangeisha haraka akachukua viatu na kuviweka ili uendelee kuungua taratibu na baada ya hapo alichukua mabaki na majibu na kupanda gari yake aina ya Subaru na kuondoka hadi shambani kwake  Morogoro ndipo alipofukia na kupanda mgomba juu ya mabaki hayo.

Jaji alisema hakuna mtu anayeweza kutoa mtiririko huo wa matukio isipokuwa tule anayejua ukweli wa tukio hilo ilivyotolea, hivyo alisema kuwa maelezo hayo ni ya kweli na ya kuaminika.

Pia alisema kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi namba nne ambaye alikuwa ni Mpwa wake ni wa kuaminika kwani hakuwa na sababu ya kumuongelea uongo mjomba kwani kwa sababu ndiye aliyemtoa kijijini kumleta Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kazi.

Baada ya mshitakiwa kukutwa ana hatia alipata nafasi ya kujitetea na katika utetezi wake alidai kuwa maelezo hayo ya onyo yalikuwa si ya kwake na jaji alisema mahakama ilitupilia mbali kwani hakukataa maelezo hayo mara ya kwanza yalipoletwa kama kielelezo mahakamani.

Alisema pia mahakama inaangalia baada ya mauaji ni kutu gani kilitendeka na kwa mujibu wa maelezo maada ya mauaji aliviringisha mwili kwenye shuka mbili na kwenda kuuchoma na kwa mujibu wa maelezo hayo inaonyesha mshitakiwa alidhamiria kutenda kosa.

Pia mawakili wa mshitakiwa walidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa akiwa hana akili timamu na alichukuliwa na kupimwa uwezo wake wa kufikiri lakini kutokana na mtiririrko ulivyojieleza mshitakiwa alionekana kuwa na akili timamu kwani aliweza kufikiria kutenda matukio yote.

Jaji alisema kuwa mahakama hiyo ilimtia hatiani mshitakiwa kwa kumuua mke wake chini ya kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya adhabu.