Tanzania na Malawi zimesaini hati ya makubaliano katika sekta ya afya na mkataba wa kuhamisha wafungwa , ikiwa ni hatua muhimu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili jirani.

Makubaliano hayo yamesainiwa tarehe 26 Februari 2025 wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) aliyeongoza ujumbe wa Tanzania alisaini makubaliano hayo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo alisaini pia makubaliano hayo.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kombo amesema kusainiwa kwa makubaliano haya ni moja ya mafanikio ya mkutano huo na ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi.

Mhe. Waziri amezihimiza taasisi na sekta husika kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa tija na ufanisi ili kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo, amepongeza hatua hiyo muhimu na kubainisha kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo ni chachu ya mabadiliko katika sekta za afya na haki za wafungwa.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo utaimarisha huduma za afya na kusaidia katika kusimamia haki za wafungwa walioko katika magereza ya mataifa hayo.

Mbali na kusainiwa kwa makubaliano hayo, mkutano huo pia umejadili maeneo mengine ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, yakiwemo biashara, elimu, miundombinu, nishati, na usalama wa mipaka.

Viongozi wa pande zote mbili wameahidi kuhakikisha kuwa uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa hayo unaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wao.

Pia, wamekubaliana kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo unapaswa kufanyika kwa wakati ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa  na kuongeza ushirikiano wa pande mbili kwa kiwango cha juu zaidi.

Mkutano huo wa JPCC ulitanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi kutoka Tanzania na Malawi uliofanyika tarehe 25 Februari 2025.