Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
JUKWAA la Uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoa wa Dodoma limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupitishwa na mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na kusema watamuunga mkono kufanikisha anapata miaka mingine mitano ya kuongoza nchi.
Pia jukwaa hilo limempingeza Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kupitishwa kuwa mgombea mwenza wa nafasi ya Urais.

Akitoa tamko hilo leo Februari 26 2025 Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Maryrobbi Mabhaya amesema kuwa viongozi na wajumbe wa jukwaa hilo wameridhika na juhudi kubwa anayofanya Rais Samia katika kuipeleka mbele nchi kiuchumi.
“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwani ameweza kusimamia suala la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kwa kupitisha kanuni ya kusimamia mamlaka ya Serikali za mitaa kuanzisha mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi unaotokana na mapato ya asilimia 10 ya mapato ndani ya halmashauri hivyo kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa masharti nafuu kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu, “amesema
Amesema kuwa Rais Samia amefanikiwa kuongezeka kwa fedha za mikopo ya wanawake,vijana na wenye ulemavu (asilimia 10)Kutoka Sh bilioni 2.5 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh. bilioni 3.3 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 32,ongezeko hilo limesaidia kuongeza idadi ya vikundi Vinavyonufaika na mikopo inayotokana na halmashauri.

Pia amesema Rais Samia amewezesha makundi maalum ya watu maskini kupitia mpango TASAF kuweza kujikimu, kupeleka watoto shake, kupata matibabu, kuanzisha miradi ya kujikwamua kwenye umaskini
Alitaja mambo mengine yaliyofanywa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara za mijini na vijijini uliorahisisha kufikika kirahisi misimu yote ya mwaka.
Mafaniko mengine ni Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unerahisisha mawasiliano kati ya Dodoma na Dar es Salaam na kuwezesha wafanyabiashara kuwa na safari za kwenda na kurudi.
“Rais Wetu amefanikiwa kujenga kiwanja cha Ndege cha kimataifa cha Msalato na kuboresha kiwanja cha ndege cha Dodoma na kuwezesha ndege kutua usiku ,”amesema
Aidha kuanzisha Samia legal aid ambayo inasaidia kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wanyonge kutatuliwa migogoro kama ya mirathi na haki nyingine za wanawake.

“Rais Samia amewezesha kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya na huduma za mama na mtoto, wanawake sasa wana uhakika wa uzazi salama, ameboresha miundombinu ya elimu kuanzia ngazi za shule ya msingi ,Sekondari,, vyuo vya kati na vyuo vikuu, “amesema.
Mabhaya amesema Rais Samia amewezesha kujenga tabia ya kuvumiliana na kusameheana, kupitia kukaribisha mashauriano na maridhiano ya makundi mbalimbali na kufanya nchi kuwa tulivu.
“Jukwaa limeunganisha nguvu za makundi yote kumuunga mkono mama kufanikisha mitano tena, “alisema.

Naye Mwajabu Nyamkomolo kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma,aliwataka wanawake kujiandaa kushiriki kongamano la wanawake kwa ajili ya maandalizi ya siku ya wanawake duniani iliopangwa kufanyika kitaifa Machi 8 jijini Arusha
Amewataka Jukwaa hilo kuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ya kijamii yanayosaidia kuchagiza maendeleo yanayofanywa katika maeneo mbalimbali.
