Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeona jumla ya wagonjwa 745,837 ambao kati ya hao watu wazima walikuwa 674,653 na watoto 71,184 wagonjwa waliolazwa walikuwa 30,645 watu wazima wakiwa 25,273 na watoto 5,372.

Hayo yameelezwa leo February 26,2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji
Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari Wagonjwa waliotibiwa katika JKCI Upanga walikuwa 513,484 kati ya hao watu wazima 470,119 na watoto 43,365 wagonjwa waliolazwa walikuwa 17,668 watu wazima wakiwa 14,580 na watoto 3,088.

Amefafanua,”Katika hospitali yetu ya Dar Group iliyopo eneo la TAZARA tumetibu wagonjwa 278,839 kati yao watu wazima walikuwa 238,570 na Watoto 40,269. Wagonjwa waliolazwa walikuwa 12,977 watu wazima 10,693 na watoto 2,284,
Huduma tulizozitoa ni za matibabu ya moyo, kinywa na meno, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na wajawazito, kliniki ya watoto, macho, pua, masikio na koo, kliniki ya ngozi, vibofu vya mkojo, upasuaji mkubwa na mdogo, magonjwa ya tumbo na ini, figo na matibabu mengine ya magonjwa yanayoambukiza kama malaria,”amefafanua

Kuhusu huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services amesema kuwa zimetolewa katika mikoa 20 na maeneo ya kazi 14 kwa watu 21,324 watu wazima wakiwa 20,112 na watoto 1,212 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Dkt. Kisenge amefafanua kuwa kati ya hao 8,873 watu wazima wakiwa 8,380 na watoto 493 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu. Wagonjwa 3,249 watu wazima 2,765 na watoto 484 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.

“Wataaamu wetu walivuka mipaka ya nchi na kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo katika nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Watu wa Comoro wakiwa katika nchi hizo walitibu wagonjwa 1,189 watu wazima walikuwa 851 na watoto 338. Wagonjwa 262 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI, “amefafanua

Aidha idadi ya wagonjwa waliotibiwa kutoka nje ya nchi amesema walikuwa 689 ambao walitoka katika nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Watu wa Comoro , Msumbiji, Nigeria, Siera Leone, Zimbabwe, Zambia, Uganda, Congo, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za Armenia, China, Ujerumani, India, Norway, Ufaransa na Uingereza.

“Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery —CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 2,784 kati ya hao watu wazima walikuwa 1,880 na watoto 904.

Upasuaji mpya wa moyo wa kufungua kifua uliofanyika ni wa kurekebisha mshipa mkubwa wa damu uliotanuka kwenye kifua na tumbo, kurekebisha valvu za moyo kwa watu wazima, kurekebisha mshipa uliotanuka kwenye bega na kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unafanya kazi bila ya kuusimamisha,”amesema

Ametaja magonjwa mengine ni kukarabati mlango wa moyo wa mshipa mkubwa wa damu iendayo kwenye mapafu kwa kutumia chumba cha moyo cha juu kulia, kutoa dawa ya kuzuia maumivu sehemu ya uti wa mgongo wakati wa upasuaji mkubwa wa moyo.

Amesema kupitia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia mionzi maalum wagonjwa 8,789 walipata huduma ya matibabu kati yao watu wazima walikuwa 7,997 na watoto ambapo wagonjwa hao walipata huduma za uchunguzi, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo.

“Wagonjwa 469 walitibiwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo kwa kutumia mtambo wa kawaida na 109 walitibiwa kwa kutumia mtambo wa Carto 3,matibabu mapya yaliyofanyika katika mtambo wa Cathlab ni upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka sehemu ya kifua na tumbo, “ameeleza

Licha ya hayo ameeleza kuwa ili wananchi wengi zaidi wafikiwe na huduma, JKCI imefungua kliniki mbili za matibabu ya moyo zilizopo Kawe katika jengo la Mkapa Health Plaza na nyingine Oysterbay katika jengo la Oyster Plaza kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima, kliniki za mishipa ya damu, huduma za maabara na huduma ya matibabu majumbani.

Nyingine ni elimu ya afya, lishe bora na mafunzo kwa jamii, huduma ya matibabu ya magonjwa ya ndani, duka la dawa, tiba mtandao, huduma ya gari la wagonjwa na huduma ya upimaji wa afya kwa vikundi mbalimbali.

“Katika kuboresha huduma za afya mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni uliogharimu shilingi milioni 526,604,116 umefungwa katika Hospitali ya Dar Group pia mtambo mwingine wa kuzalisha hewa ya oksigeni wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 umefungwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), “amesema