*Awaasa Wanamsalala kuchagua maendeleo badala ya maneno

*Rais Samia atakeleza Ilani ya CCM kwa 99% Msalala

*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa angependa kuona wananchi wa Kahama wanashirikiana na kuungana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo ya Wilaya yao.

Aidha, amewaasa kutoacha msingi wa Chama Cha Mapinduzi wa kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba Taifa linategemea CCM iwahudumie na sio kuruhusu mipasuko miongoni mwao.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Februari 25, 2025 Kahama, mkoani Shinyanga wakati aliposhiriki katika Mkutano Maalum wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Msalala uliolenga kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025.

Akizungumzia fursa za maendeleo zilizopo wilayani humo, Dkt. Biteko amesema kuwa Kahama ni Wilaya ya kimkakati ambayo ina bandari kavu iliyopo Isaka ambapo pia kitajengwa kiwanda cha kuchenjua madini pamoja na uwepo wa barabara inayoounganisha nchi za maziwa makuu.

“ Kutokana na uwepo wa fursa hizi tukishindwa kuungana tukashughulika na maendeeo ya watu basi watatushangaa. Nataka nitoe wito, pendaneni, shikamaneni Mungu amewapa kila aina ya utajiri tumieni fursa hiyo kujiletea maendeleo kwenye wilaya yenu na msiruhusu mipasuko katika chama chetu,” amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza “Nawaomba baada ya mkutano huu tutoke hapa tukiwa wamoja na tuweke mbele maslahi ya Chama chetu na watu wetu,”

Pia, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Msalala, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanapata miradi ya maendeleo na hivyo kutatua changamoto walizokuwa nazo hapo awali.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi katika Jimbo hilo ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali kama vile ya maji, elimu, afya na miundombinu.

“ Mhe. Rais Samia amefanya makubwa katika nchi yetu, leo tunazungumza kuhusu miradi mingi na mikubwa hapa Kahama, tunazungumzia kujengwa kwa barabara ya Kakola kwa kiwango cha lami. Amefanya uchimbaji madini ubaki kwenye maendeleo yetu anataka uwepo wa miradi mingi zaidi ya barabara na maji niwaombe tumuombee ili aendelee kutimiza haya kwa ajili ya Watanzania,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia bado ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata maendeleo na kuishi katika mazingira bora zaidi.

“ Wito wangu kwenu shikamaneni, pendaneni, vumilianeni tukijenge Chama chetu ikiwa muda utafika wakati wa uchaguzi basi chagueni anayefanya kazi mwacheni anayesema watu. Mhe. Mbunge Iddi endelea kuchapakazi kwa maendeleo ya Jimbo lako.” Amemalizia Dkt. Biteko.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Msalala lililopo Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Iddi Kassim Iddi wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Jimbo hilo kwa Mwaka 2020 hadi 2025 amempongeza Dkt. Biteko kwa hatua ya kuendeleza sekta ya nishati kwa kusaidia vitongoji vyote vya Jimbo hilo kupata umeme.

Serikali inaendelea na azma yake ya kusambaza huduma za umeme katika vijiji vyote nchini. Hapa tumejulishwa kuwa Msalala ina jumla ya vijiji 92, ambavyo vyote vimefikiwa na huduma ya umeme, kazi iliyobaki ni kupeleka umeme katika vitongoji.

Akizungumzia sekta ya maji amesema mwaka 2020 hadi 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mfano ametoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya miradi ya kusambaza maji katika vijiji mbalimbali.

Ameendelea kusema mafanikio ya miradi hiyo imesaidia Jimbo hilo ambalo kwa sasa wanaendelea kusambaza maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo hususan katika vitongoji na tayari Serikali imeshaleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“ Wakati naingia madarakani miradi ya maji ilikuwa kwa asilimia 25 pekee na sasa miradi ya maji imefikia asilima 95,” amesema Mhe. Iddi

Kwa upande wa sekta ya elimu amesema kuwa Rais Samia ameboresha sekta hiyo kwa kutoa fedha zilizosaidia katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa, mabweni na maabara.

“ Tumekuwa na shule nyingi maana yake tutawasomesha watoto wetu kwa kiwango cha kutosha, pia tumeanzisha ujenzi wa Chuo cha VETA na kitakapo kamilika kitakuwa na manufaa makubwa kwa jamii hususan vijana ili wapate ujuzi na kuajirika katika soko la ajira,” amesema Mhe. Iddi.

Halikadhalika katika sekta ya barabara amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano Jimbo hilo kwa kushirikiana na TARURA wamefungua barabara nyingi ikiwemo barabara inayotoka Kakola kwenda Kahama ambayo kwa sasa inapitika vizuri. Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kutekeleza Ilani ya CCM katika Jimbo hilo kwa asilimia 99.9 .