Na Magrethy Katengu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

BONDIA Amiri Matumla,anatarajia kupanda ulingoni Februari 28, mwaka huu, kupambana na mpinzani wake kutoka Namibia, Paul Amavila.

Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo, Feb 25, 2025 na Mkurugenzi wa Mafia Boxing Promotion, ‘Knock Out ya Mama’ Ally Zayumba na kufafanua kwamba bondia huyo katika pambano hilo atazichapa na mpinzani wake kwa mizunguko nane katika ukumbi wa Magomeni Sokoni.

‘Hili ni pambano lake la kwanza tangu ajiunge kwenye mapambano ya ngumi za kulipwa na ameahidi kufanya vizuri kwa lengo la kuanza kutenge rekodi nzuri katika karia yake kupitia masumbwi,” amesema.

Zayumba ameongeza kwamba siku hiyo pambano hilo kutakuwa na mapambano mengine 11 ya utangulizi yakiongozwa na mkongwe Dullah Mbabe.

Pia amesema kuwa huu ni msimu tatu Kwa mapambano ya aina hiyo kufanyika chini ya Mafia Boxing Promotion yakiwa na lengo la kunadi miradi iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amefafanua kwamba michezo wa ngumi katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Dkt Samia, umekuwa na mafanikio makubwa hivyo ni vema watanzania wakaendelea kumuunga mkono.

Pia amesema viingilio vitakuwa ni shilingi, 50,000, sh. 20000 na 10,000 na mabondia wote watapima uzito katika Ukumbi huo Feb 27, mwaka huu.

Zayumba ametaja mabondia wengine watakaopanda ulingoni katika mapambano ya utangulizi ni Oscar Richard atakayezipiga na bondia kutoka Malawi.

Rashid Mtange kutoka Nacoz Camp chini ya kocha Ramadhani Uhadi ‘Rama Jah’ atazichapa na bondia kutoka India na wengineo.

Naye Bondia Matumla, ambaye ni mtoto wa Rashid Matumla’ Snake Man’ amejinasibu kufanya vizuri pambano hilo kutokana na kupata maandalizi ya kutosha.

‘Naomba watanzania wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia pambano hilo ambalo litakuwa na burudani ya aina yake, amesema.