Polisi Rukwa kuwasaka waliofukua kaburi na kuondoka na mwili wa marehemu
JamhuriComments Off on Polisi Rukwa kuwasaka waliofukua kaburi na kuondoka na mwili wa marehemu
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa
Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linawatafuta watu waliohusika kufukua kaburi la Julius Ladislaus (24) aliyefariki Novemba mwaka jana na kuondoka na mwili wa marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Shadrack Masija amesema kuwa marehemu alifariki Novemba mwaka jana wilayani Chunya mkoani Mbeya na mwili wake kusafirishwa mkoani Rukwa na kuzikwa katika Kijiji cha Lunyala wilayani Nkasi.
Amedai kuwa mnamo Februari 14, 2025 mwili wa marehemu ulikutwa umefukuliwa na kuliacha sanduku na kaburi lake vikiwa wazi .
Hivyo amewaomba wananchi wote walio na taarifa juu ya watu waliofanya vitendo hivyo viovu na vya kutisha kutoa taarifa Polisi ili watuhumiwa waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kamanda Masija Alidai kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina juu ya suala hilo na kuwa kimsingi suala hilo linahusishwa na imani za kishirikina na kuwasihi wananchi kuacha a na imani hizo ambazo katika kipindi hiki zimepitwa na wakati.