Na Magrethy Katengu, JamuhuriMedia,
Dar es Salaam
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kipaumbele chake kwa sasa ni kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini utakaoleta haki, kuheshimiwa maamuzi na matakwa ya wananchi.
Ameyasema Februari 24, 2025 Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu wakayo akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo amesema maazimio ya Halmashauri Kuu ya Chama iliyokutana jana imeelekeza katika suala la kushiriki ama kutoshiriki uchaguzi kabla ya kufanyika marekebisho yanayotakiwa litaamuliwa na Kamati ya Uongozi ya Taifa katika wakati muafaka,
Hata hivyo Shaibu amefafanua hayo ikiwa ni moja kati ya maazimio saba ya Halmashauri Kuu, ambapo amesema azimio la pili ni kuwa Halmashauri Kuu ya Chama imejiridhisha kuwa maridhiano yaliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan yamesambaratika na falsafa yake ya 4R imeota mbawa.

Sambamba na hayo amebainisha kwamba Chama cha ACT Wazalendo, vyama vingine vya upinzani na wadau wengine wa demokrasia nchini walimuunga mkono Rais Samia kutokana na ahadi yake ya kuboresha mazingira ya kisiasa nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba chaguzi zinakuwa huru, za haki na za kuaminika.
Kwamba Halmashauri Kuu imejiridhisha kuwa hakukuwa na utashi wa kisiasa kutekeleza ahadi hii.
Hata havyo , Halmashauri Kuu imemtaka Rais Samia kujitathmini juu ya tofauti iliopo baina ya ahadi anazotoa kwa maneno na kukosekana kwa vitendo katika kutekeleza ahadi hizo.
Kuhusu azimio la tatu, ameeleza, Halmashauri Kuu imeelekeza chama kifanye uchambuzi na kuandaa ripoti ya kina juu ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu nchini vilivyofanywa na vinavyoendelea kufanywa akidai kuwa vinafanywa na Serikali za Chama cha Mapinduzi (Serikali) yakiwemo matukio ya mauaji na utekaji na madhila ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Kwa upande wa Zanzibar, ACT Wazalendo kinayo ripoti ya kina juu ya mauaji ya raia 21 na matukio mengine ya ukatili wa kutisha yaliyofanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambapo pia, chama kimekusanya vitendo vyote vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu Zanzibar tangu mwaka 2020-2025.
Hivyo azimio la nne ni kuwa Halmashauri Kuu imeelekeza Ripoti hizo zichapishwe na kupelekwa kwa wadau wa demokrasia nchini pamoja na jumuiya ya kimataifa ikiwemo taasisi za fedha za kimataifa na pia kushirikiana na taasisi hizo kufikisha kesi katika Mahakama za Kimataifa.
Azimio la tano ni, Halmashauri Kuu imeelekeza kuwa Chama cha ACT Wazalendo kiendeleze ushirikiano na vyama vingine makini vya upinzani na wadau wengine muhimu wa demokrasia ikiwemo asasi za Kiraia na viongozi wa dini katika kujenga vuguvugu la kitaifa la kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini.
Katibu Mkuu Shaibu ameendelea kusema azimio la sita ni, Halmashauri Kuu imeelekeza Chama kiandae operesheni kubwa ya kulinda demokrasia nchini Tanzania itakayojulikana kama OPERESHENI LINDA DEMOKRASIA ambayo lengo la operesheni hiyo ni kuhamasisha umma wa Watanzania kupigania haki zao na kutokubali kuwa wanyonge.
Kwamba azimio la saba, Halmashauri Kuu imeelekeza chama kijikite katika kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini ikiwemo kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba (minimum constitutional reforms), kuundwa kwa Tume Huru za Uchaguzi (NEC na ZEC kwa upande wa Zanzibar) na kupinga kwa nguvu zote kura ya mapema kwa upande wa Zanzibar.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wanachama na viongozi kwenye ngazi zote kujiandaa kwa ajili ya mapambano ya kuilinda na kuitetea demokrasia nchini ili kura ya kila mwananchi iweze kuwa na thamani.