Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuweka Jiwe la msingi la ujenzi wa Bwawa la Mkomazi pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi wa Skimu za Mkomazi na Chekelei Wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Kwa Mujibu wa Taarifa kwa Vyombo vya Habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa imeeleza kuwa hafla hiyo itafanyika wilayani Korogwe Februari 24 Mwaka huu.
Mradi wa Mkomazi ni wa kihistoria, uliobuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu.

Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua Umuhimu wa Mradi huo imetoa shilingi Billioni 18 kwa ajili ya Kugharamia utekelezaji wake.
Zaidi ya wakulima elfu 20 kutoka Vijiji 28 vya kata saba za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni na Magila Gereza Wilayani Korogwe wanatarajia kunufaika na Mradi wa Mkomazi.

Mradi huo unaotarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025,Utahusisha ujenzi wa tuta la udongo la kuzuia maji, ujenzi wa barabara kuelekea eneo la mradi na ujenzi wa ofisi ya meneja wa mradi.
Mbali na kuweka Jiwe la msingi la ujenzi wa Bwawa la Mkomazi,Rais Samia pia atashuhudia utiaji saini Mkataba wa ujenzi Skimu ya Mkomazi yenye Jumla ya Hekta 9,000.
Skimu hiyo ambayo Ujenzi wake utagharimu shilingi Billioni 48.3 itahudumia Vijiji 28 vya kata saba za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni na Magila Gereza Wilayani Korogwe.
Vilevile, Rais atashuhudia utiaji saini wa mkataba wa mradi wa Chekelei ambao ni ujenzi wa bwawa na skimu yenye ukubwa wa hekta 1049 ambayo itagharimu Billioni 31.2 na inakusudia kuwanufaisha wananchi vijiji vinne vya Madala, Madumu,chekelei na Chepete.
“Tuna imani kuwa miradi hii itachochea maendeleo na kuboresha maisha ya wakazi wa Korogwe na maeneo jirani,Tunawashukuru wote kwa ushirikiano na tunawaomba muendelee katika juhudi hizi za kimaendeleo, kupitia kilimo cha Umwagiliaji” Ilieleza sehemu ya Taarifa
ya Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa.
