Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kupeleka zaidi ya sh bil 51 katika halmashauri ya manispaa Tabora kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo tangu mwaka 20201.
Kiasi hicho kimepelekea miundombinu ya huduma za kijamii kufanyiwa maboresho makubwa hivyo kuwezesha wakazi wa manispaa hiyo kupata huduma bora za kijamii katika sekta mbalimbali tangu Rais Samia aingie madarakani.
Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Shaban Kapela alipokuwa akifungua kikao cha robo ya pili ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo juzi.
Alieleza kuwa kati ya fedha hizo kiasi cha sh bil 7.3 zimetumika kutekeleza miradi ya afya, sh bil 9.4 miradi ya elimu kwa shule za msingi na sh bil 23 kwa shule za sekondari ambapo shule mpya za sekondari zimejengwa katika kata zote.
Aidha kiasi cha sh bil 5 zilitumika kwenye shughuli za utawala huku zaidi ya sh bil 2.5 zikitumika kuinua sekta ya kilimo ikiwemo kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu kwa wakulima ili kuboresha shughuli zao.
Mstahiki Meya aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 4 ya uongozi wa Rais Samia wamepokea zaidi ya sh bil 3.8 kwa ajili ya uhawilishaji kaya maskini hali iliyopelekea vijana, akinamama na watu wenye ulemavu kuinuliwa kiuchumi.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 4, serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefikisha huduma ya umeme katika vijiji 12, 301 kati ya vijiji 12,318, vimebakia vijijij17 ambapo utekelezaji unaendelea.
Kwa upande wa Vitongoji, Kapela alisema kuwa hadi sasa zaidi ya asilimia 60 ya Vitongoji vyote vimeshafikishiwa huduma hiyo na wananchi wameendelea kunufaika kwa kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Diwani wa Kata ya Gongoni katika manispaa hiyo Kessy Sharif Abdulrahman aliunga mkono tamko hilo na kuitaka halmashauri kusimamia ipasavyo miradi yote iliyoanza kutekelezwa ili ikamilike haraka na kwa wakati kwa faida ya wananchi.
‘Serikali ya awamu ya 6 imefanya kazi nzuri sana katika halmashauri yetu, naomba miradi ambayo haijakamilika isimamiwe ipasavyo ili ikamilike kwa wakati, hususani ujenzi wa matundu ya vyoo katika baadhi ya shule’, alisema.
Naibu Meya Mstaafu wa Manispaa hiyo Rose Kilimba (diwani wa Kata ya Ifucha) alipongeza maboresho makubwa ya huduma za kijamii yaliyofanywa na serikali ya awamu ya 6 katika kata yake na manispaa nzima.
Aliomba wakazi wa Mitaa ya Tuli, Usuhilo na Miziwaziwa katika kata yake wapimiwe maeneo yao na kumilikishwa ili wasisumbuliwe na matapeli wanaouza ardhi kinyemela.
