Juhudi za utawala wa Rais Donald Trump katika kuimarisha usalama wa taifa na idara za usalama zimepiga hatua muhimu baada ya Seneti kupiga kura ya kuidhinisha uteuzi wa Kash Patel kuwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Marekani (FBI) na alishinda kwa kura 51-49.

Hivyo ushindi huo unamuweka Patel kwenye uongozi wa idara hiyo yenye nguvu, ambapo awali aliahidi kuleta mabadiliko wakati wakosoaji wa Rais wa Marekani Donald Trump wakisema kuwa utawala wake unahujumu utamaduni wa uhuru wa idara hiyo.

Warepablikan wawili –Seneta Susan Collins na Lisa Murkowski, walipiga kura na Wademokrat wakipinga kuidhinishwa kwa Patel. Hata hivyo uungaji mkono kutoka kwa Warepablikan wengine ulimpatia Patel ushindi mdogo, wengi wao wakimsifia na kusema kuwa ataleta mabadiliko.

“Wamarekani wengi katika miaka ya karibuni wamepoteza imani yao kwa FBI, sababu kubwa ikiwa ni dhana kwamba siasa zimeingilia majukumu yake muhimu,” alisema kiongozi wa walio wengi kwenye Seneti John Thune, muda mfupi kabla ya kupiga kura.

Thune aliongeza “Tunahitaji idara inayofanya kazi pamoja kushughulikia tishio dhidi ya nchi yetu,” Pia amesema kuwa yupo tayari kushirikiana na Patel ili kuhakikisha kuwa FBI inatekeleza majukumu yake ipasavyo. Baadhi ya Warepablikan wenzake pia wametoa maoni sawa na hayo.