Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

SERIKALI imeanza maandalizi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vinane vya ubunifu katika mikoa minane ili kuboresha mazingira ya watafiti na wabunifu wa TEHAMA nchini.

Aidha Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua kampeni ya” Sitapeliki ” yenye lengo la kuhakikisha wananchi hawatapeliwi na matapeli bali watawasiliana na kampuni za watoa huduma kupitia namba 100 pekee.

Hayo yamesemwa leo jiijini Arusha na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano na teknolojia ya Habari kuhusu utekelezaji wa mkakati wa taifa wa uchumi wa kidigitali 2024/25

Mhe.Silaa ametaja mikoa hiyo kuwa ni  Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya, Tanga, Lindi, Zanzibar na Mwanza lakini pia vituo  hivyo pia vitawezesha ujenzi wa vyuo viwili vya umahiri vya Tehama ambayo vinajengwa Dodoma eneo la (Nala) na Kigoma (Buhigwe)  huku taratibu za ujenzi  zikiendelea.

Amesema vyuo hivyo ni  mahususi kwa utoaji wa ujuzi kwa vitendo hivyo mitaala yake itakuwa ya kumuwezesha mwananchi kupata ujuzi na kuweza kujiajiri vijana

Ameongeza kuwa, katika kuelekea uchumi wa kidigitali serikali kupitia wizara hiyo imeratibu ujenzi wa mfumo wa kitaifa wa kuunganisha mifumo yote ya Tehama nchini ijulikanayo kama “Jamii X-Change” ambapo jumla ya mifumo 898 imeunganishwa katika miundombinu 14 ya kubadilisha taarifa ambapo  mifumo 514 ni ya serikali huku mifumo 384 ni ya sekta binafsi lakini pia mifumo ya jamii namba na jamii malipo imetengenezwa kwa ajili utambuzi na huduma za malipo “cashless”.

Aidha  kikao kazi hicho kimeenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kushughulikia masuala ya utapeli mtandaoni iitwayo “SITAPELIKI” imezinduliwa rasmi ikiwa mkakati wa serikali pamoja na watoa huduma za simu na intaneti kunusuru wateja.

Aidha Kampeni hiyo imezinduliwa leo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari.

Amesema kuwa ,kampeni hiyo ya ” Sitapeliki ” ina  lengo la kuhakikisha wananchi hawatapeliwi na matapeli bali watawasiliana na kampuni za watoa huduma kupitia namba 100 pekee.

Ameongeza kuwa,kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na kuwapa wananchi maarifa zaidi ya jinsi ya kujikinga dhidi ya majaribio mbalimbali ya ulaghai na hatimaye kujiepusha na udanganyifu unaofanywa na watu wachache wenye lengo la kujinufaisha.

Katibu mkuu wa wizara hiyo Mohamed Abdulla amesema kikao kazo hicho kimelenga kutathimini utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidigitali wa miaka 10 kuanzia 2024hadi 2034.

Amesema kuwa mkakati huo utakuwa na nguzo sita za kuwezesha miundombinu ya kidigitali, utawala na mazingira wezeshi ,uelewa wa kidigitali na maendeleo ya ujuzi ,utamaduni wa ubunifu wa kidina teknolojia wezeshi.

Aidha ameongeza kuwa,nyingine ni pamoja na kukuza ushirikishwaji wa kidigitali na ufikishaji wa huduma za kifedha za kidijitali.