Rais wa Marekani Donald Trump amemuita Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine dikteta anayekataa kuitisha uchaguzi na kumuonya kwamba anabidi kuchukua hatua za haraka kutafuta amani au kupoteza nchi yake.

“Amekataa kufanya uchaguzi, hana umaarufu katika kura za maoni ya Waukraine wenyewe. Unawezaje kuendelea kuwa juu, huku kila mji umeharibiwa? Ni vigumu sana….kuna mtu anasema, hapana bado umaarufu wake uko juu. Tafadhali, niache.” Alisema Trump

Kauli ya Trump ya kumshambulia Zelensky imetolewa siku moja baada ya kiongozi huyo wa Marekani, kudai kwamba Ukraine inapaswa kulaumiwa kuhusu uvamizi uliofanywa na Urusi mwaka 2022.

Rais Zelensky alikataa kwenda Riyadh kujadili na Urusi na Marekani kuhusu amani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha, badala yake amesema hakuna anayeweza kuifanya nchi hiyo kusalimu amri.

Mtazamo wa Trump umeleta wasiwasi miongoni mwa washirika wa Marekani barani Ulaya, kwamba mwelekeo wa kiongozi huyo wa kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine huenda ukawa na maslahi zaidi kwa Urusi.