Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mbio za Samia Marathon zitakazofanyika Februari 22, 2025, katika viwanja vya Shule ya Mtongani, Mlandizi, Kibaha Vijijini, mkoani Pwani.

Mbio hizi zinalenga kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kupiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mbio hizo kwa waandishi wa habari ofisini kwake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoani Pwani, Josian Jackson Kituka, alisema kuwa Samia Marathon imeandaliwa na Jumuiya hiyo ya Mkoa na maandalizi yake yamekamilika.

Alieleza kwamba lengo kuu la mbio hizo ni kuhamasisha watu kujenga tabia ya kupiga kura wakati wa chaguzi, kwani wengi wao wamekuwa wakijiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lakini wanashindwa kupiga kura wakati wa uchaguzi.

Josian alifafanua ,Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa ya kuinua uchumi na maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla, hivyo zoezi la kujiandikisha limekamilika na kilichobakia ni wananchi kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Kwa mujibu wa Josian, matarajio yao ni kuwa wananchi pamoja na viongozi takriban 7,000 watashiriki katika shughuli hiyo kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Morogoro, Zanzibar, na Dar es Salaam.

“Hii ni mara ya kwanza kwa Jumuiya yetu ya Wazazi mkoa wa Pwani kuandaa tukio kubwa kama hili, Tunawaomba wananchi wajitokeze Jumamosi, Februari 22, Mlandizi kuanzia saa 1 asubuhi kuunga mkono jambo hili,” alisema Josian.

Sambamba na mbio hizo kutakuwa na matukio mengine ikiwa ni pamoja na sanjali, kuvuta kamba, kuendesha baiskeli, kutembea umbali wa km 5, na burudani za muziki.