Mkutano wa mawaziri wa masuala ya kigeni wa nchi tajiri duniani (G20) umeanza leo huko Afrika kusini.

Hata hivyo, Marekani kupitia Waziri wake wa masuala ya kigeni wa Marekani Marco Rubio haitohudhuria mkutano huo.

Marco Rubio alitangaza kutohudhuria kupitia kwenye mitandao ya kijamii mapema mwezi huu akitaja kuwa ‘’Afrika kusini inafanya mambo ya kutamaushwa’’, akielezea kuwa jukumu lake ni kupigania maslahi ya Wamarekani na sio kufuja kodi wanazozitoa.

Trump alifuta misaada kwa Afrika Kusini akijibu mswada wa unyakuzi uliotiwa saini hivi majuzi ambao unaweza kuruhusu serikali kutwaa ardhi bila fidia.

Pretoria imekanusha mara kwa mara kwamba kuna unyakuzi wowote kiholela wa ardhi au mali ya kibinafsi nchini Afrika Kusini.

Tamko hilo limeendelea kuweka uhusiano wa kidiplomasia baina ya Afrika kusini na Washington njia panda haswa wakati huu wa utawala mpya wa Rais Donald Trump.

Huenda lengo la mkutano halitaafikiwa ambapo Afrika kusini walitaka kuutumia kukuza masuala muhimu kwa nchi zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha za maendeleo na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Huu ni mkutano wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi la G20 yenye uchumi mkubwa tangu Afrika Kusini ilipochukua nafasi ya urais mwezi Disemba mwaka jana.