Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mambo makubwa yanayohusu hatima ya taifa letu hayana budi yasemwe hata kama kufanya hivyo kutaleta gharama kwa wanaoyasema.
Huu ni wajibu wa kikatiba, kwa kuwa wananchi wa Tanzania, kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, tunayo haki ya kushiriki katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa letu.
Huu ni ulinzi mtambuka; kuna ulinzi wa viongozi na mamlaka za nchi na ulinzi wa kijamii, ambao wengi wetu, bila madaraka yoyote ya kisiasa, tunapaswa kuutekeleza kwa njia ya kutoa taarifa na kuibua mambo ambayo yanaonekana kuathiri rasilimali hizo.
Ni vigumu sana kwa rais, mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wa serikali kuwa na taarifa kamili ya kila kitu kinachotokea katika sekta muhimu kama hizi za uhifadhi na utalii.
Sekta hizi zina mchango mkubwa kwa uchumi wetu, na kama hatutazungumza yale yanayojiri katika maeneo ya uhifadhi, tunaweza kushuhudia sekta hizi zikishindwa kustawi na kuleta madhara kwa taifa letu. Hali hiyo inaweza kutokea ikiwa sisi, wananchi, tutakaa kimya kwa sababu ya woga, unafiki au kutojali, huku tukiacha matatizo yakiendelea kuzorotesha mambo.
Yanayoendelea kwenye sekta hii yasiposemwa; kwamba sote tukiamua, ama kwa woga, au kwa unafiki kukaa kimya, sekta hii inayoongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni itatoweka.
Bahati mbaya tumekuwa na ugonjwa huu wa kusifu na kudanganyana. Tunaamini kusema ukweli kunatuondolea marafiki, kunatuondolea maisha yetu mazuri; na pengine kunatufanya tutengwe.

Sasa tunapozungumzia taasisi muhimu za uhifadhi, kama vile Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), tunazungumzia taasisi ambazo zina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa taifa letu, lakini pia kwa faida kubwa za kiuchumi na kijamii.
Mapori yetu yana mchango mkubwa katika kuchangia mapato ya fedha za kigeni, kutoa maji na kutoa huduma za kimazingira. Hivyo ni muhimu kuzielewa changamoto zinazoyakumba.
Kwa miezi kadhaa iliyopita, nilielezea kuhusu hujuma zinazofanywa katika maeneo ya mashariki mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti, na magharibi mwa Pori la Akiba Pololeti, ambako ujangili unakua na kuleta athari kubwa kwa wanyamapori na mazingira. Inasikitisha kuona kwamba hali ya ujangili inazidi kuongezeka, na majangili wanashirikiana na baadhi ya watumishi wa serikali.
Hii ni changamoto kubwa kwa uhifadhi wetu, na hali hii inadhihirika katika tukio la hivi karibuni la kufukuzwa kwa askari wa TANAPA ambao walihusishwa na kupokea rushwa ya Sh milioni 500 ili kuruhusu mifugo kuingizwa katika Hifadhi ya Burigi-Chato.
Tatizo hili si la Burigi-Chato pekee, bali ni la maeneo yote yanayohifadhiwa. Ujangili wa wanyamapori kwa ajili ya kitoweo uko juu, kadhalika hata ujangili wa wanyama adhimu.
Hali hii inatulazimu tujiulize maswali muhimu: Kwa nini wataalamu hawa wanaokuwamo kwenye taasisi za uhifadhi hawatoi taarifa kuhusu ujangili na mifugo inayoingizwa kwenye maeneo ya hifadhi?
Je, kuna kizuizi cha kimfumo kinachowazuia kusema ukweli kuhusu hali ya uhifadhi? Je, ni kwa sababu ya woga, au wanadhani kuwa kudhihirisha ukweli kutawatenga au kuchukuliwa hatua kali?
Tujiulize, kwa nini sasa si TANAPA, NCAA, TFS wala TAWA wanaotoa taarifa za ujangili na watu wanaoingiza mifugo hifadhini?
Tunasema kuwa uhifadhi ni jambo la kikatiba, lakini pia linahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali na wananchi. Hata hivyo, kuna hali mbaya inayojitokeza katika mfumo wa fedha za OC (Operating Costs), ambako fedha zinazopatikana kwa ajili ya utendaji wa taasisi hizi nyingi hazifikii malengo yake.
Hizi fedha nyingi hazielekezwi katika kutatua matatizo ya uhifadhi, bali mara nyingi hutumika kwa malengo yasiyo na manufaa kwa uhifadhi, kama vile matamasha na shughuli za utalii ambazo hazina tija kwa wanyamapori wala mazingira.
Mfumo huu wa kifedha umesababisha matatizo zaidi, kwani baadhi ya watumishi wa chini, wakiwamo askari wa Jeshi la Uhifadhi, wanashindwa kupata motisha na posho za kufanya kazi kwa ufanisi. Hali hii inaathiri morali ya watumishi hawa na inachangia kuzorotesha mambo.
Watumishi hawa wanapojikuta katika mazingira magumu, huku wakiwa na familia zinazowategemea, wanajikuta wakikata tamaa na kujiingiza katika vitendo vya rushwa au kushirikiana na majangili kwa lengo la kujilipa.
Hawa makamishna wa Uhifadhi (CCs) wa TANAPA, NCAA, TFS na TAWA kwa hali ilivyo hawastahili lawama. Taasisi zao zinaendeshwa kwa mfumo wa kijeshi, hivyo hawana mamlaka wala uthubutu wa kuyasema yanayowasibu. Kanuni za utumishi zinawafanya wafe kisabuni.
Kutokana na hali hii, inakuwa wazi kwamba mifumo ya kiutawala na kifedha inahitaji kubadilishwa ili kuhakikisha kuwa fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, na kwamba watumishi wa uhifadhi wanapata motisha ya kutosha kufanya kazi zao kwa ufanisi. Tunahitaji kuzingatia kuwa, bila uhifadhi, hakuna utalii wa kweli, na bila utalii, hatuwezi kuingiza mapato makubwa kutokana na sekta hii.
Swali la kujiuliza, kwa nini hali ni mbaya? Nitaanza na fedha. Mfumo wa OC uliopo sasa si mbaya, maana unaratibiwa kutokana na maombi yanayotokana na bajeti ya kila taasisi. Mathalani, taasisi haiwezi kuomba Sh bilioni 10 kwa mwezi halafu ikapelekewa Sh bilioni 6 pekee, kisha itarajiwe mambo yaende vizuri.
Nimeuliza mara kadhaa kama hayo mafungu wanayoomba huwa wanayapata? Sehemu kubwa ya majibu ni ndiyo, wanayapata. Kama wanayapata, fedha zinaishia wapi?
Upo ushahidi wa kimazingira kwamba mara kadhaa fedha hizi zikiingizwa benki hutolewa maelekezo zikachepushwa kwenda kufanya kazi zilizo nje ya mfumo wa maombi ya OC. Hili ni la vyombo vya uchunguzi. Muhimu na kubwa lipo.
Fedha hizi za OC ndizo huchepushwa na kupelekwa kwenye matamasha mengi ya utalii. Matamasha haya yanatumia mamilioni ya fedha kulipia kumbi, posho za wakubwa na mambo ambayo hayana tija yoyote.
Pesa hizi inadaiwa ndizo zinazotumika kuandaa mabango yenye picha na maandishi kwa shughuli hata iliyostahili ifanywe ndani ya chumba cha mikutano cha kawaida kabisa.
Kwa kuwa mfumo wa TFS, NCAA, TAWA na TANAPA ni wa kijeshi, hakuna CC yeyote kati ya hawa mwenye jeuri ya kupinga au kuhoji. Wanapopewa maelekezo wanatii kama askari. Dhana hii haifai na ndiyo maana watangulizi wa ujenzi wa mifumo waliona wahasibu kwenye majeshi wawe raia, maana hao wana jeuri ya kuhoji.
Matokeo ya kuingiza mikono kwenye OC kumefanya uendeshaji wa taasisi hizi uwe mgumu kweli kweli. Wakuu wa hizi taasisi wanalia, lakini wanalilia pembeni tu.
Waliapa kwa vitabu vya dini zao, wajitokeze hapa waseme mbele ya Mungu kuwa hali ya fedha kwenye taasisi zao ni nzuri! Nayasema haya kwa sababu baada ya andiko hili huenda wakatishwa ili wakanushe ukweli huu ingawa dhamiri zao zitakuwa zikikataa.
Ukosefu wa fedha umesababisha watumishi wa chini wakose posho na motisha kama ilivyokuwa zamani. Zama zile askari waliokamata jangili walipewa motisha. Waliokamata nyaya za mitego walitambuliwa na wakatuzwa. Waliposhinda kesi, walipewa ‘asante’ kwa kazi nzuri.
Watu hawa ambao wengi ni vijana, wanafanya kazi katika mazingira magumu mno. Wanawakwepa majangili, wanakwepa wanyama wakali, wakakabiliana na nyoka wa kila aina, wanakwepa mitego ya nyaya na mashimo ili wasinaswe kama wanyama, wanatembea kuvuka mito na maziwa kufika maeneo yasiyofikika kwa magari. Wanakesha kwenye mashimo wakilinda rasilimali hii adhimu inayoingiza mabilioni ya dola na shilingi.
Vijana hawa wameacha ujana wao na kukubali kuishi maisha ya upweke maporini. Hawajui disko wala vijiwe vya kufurahi pamoja na vijana wenzao. Kila dakika moja kwao ni dakika ya uhai au kifo.
Watu hawa wanaohangaika kulinda utajiri wote huu wamo wasio wastahimilivu. Kukosekana posho na motisha kumewashusha morali. Baadhi wamejikuta kwenye kutekeleza msamiati wa ‘tunajilipa’. Kujilipa huko ndiko baadhi yao sasa wanakofanya kwenye ujangili na uingizaji mifugo hifadhini.
Wapo wengine wanaojilipa kwa kuruhusu wageni kutoka Kenya kuingia Pololeti na Serengeti, hasa kufanya utalii wa usiku. Tunayasema haya kwa sababu wenye dhamana ya kuyasema wameamua wawe kimya.
Doria hazifanywi, na pale zinapofanywa ni kwa kuotea tu – ujanja ujanja waonekane wapo. Magari kadhaa hayana mafuta na vipuri. Haya wakubwa serikalini hawaambiwi maana wengine wetu tumechagua kusema ‘mazuri tu’.
Zile hifadhi zilizoko ukanda wa magharibi ni malisho ya Wanyarwanda wanaosaidiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa.
Ijulikane kuwa kama ilivyo kwenye mnyororo wa fedha za OC, huku kwenye ujangili na malisho hifadhini nako kuna mnyororo wa aina hiyo hiyo. Askari wachache wasio waaminifu wanashirikiana na watumishi walio ndani na nje ya hizi taasisi. Wanatoa ramani na nywila kwa majangili.
Nini kifanyike? Mosi, sisi tunaoupenda na kuuishi uhifadhi tukiri ukweli huu kwamba hali ya hifadhi zetu ni mbaya. Taasisi hazina fedha. Ujangili upo, tena upo kwa kiwango cha juu.
Pili, bila uhifadhi hakuna utalii. Kilichopo sasa ni matamasha mengi mno ya utalii, lakini si ya uhifadhi. Tuanze na ulinzi wa uhifadhi.
Tatu, fedha za OC zitolewe kwa muda na zitumike kwa kazi zilizokusudiwa kulingana na maombi ya taasisi. Pesa za OC ambazo zinapita benki zitazamwe na ijulikane zinaingia ngapi na hizo taasisi nne zinaachiwa nini. Ijulikane hizi taasisi zinalazimishwa kuchangia mambo gani yaliyo nje ya OC zao, maana haiwezekani, kwa mfano, watu waamke asubuhi watakiwe walipe posho za wajumbe, ikijulikana kabisa hizo fedha haziko kwenye bajeti.
La, hilo haliwezekani, taasisi hizi, kama ilivyokuwa awali, zipewe mamlaka ya kukusanya, kutumia na kupeleka ziada serikalini. Hili la pili litakuwa baya zaidi endapo wale wanaoingiza mikono kwenye OC sasa wataendelea kufanya hivyo.
Tatu, uendeshaji wa taasisi hizi – TANAPA, NCAA, TFS na TAWA – usiwekewe mikono ya kisiasa. Taasisi zote hizi kwa sasa zimeondolewa wataalamu wengi wa uhifadhi na kupelekwa watu wa taaluma nyingine.
Taasisi hizi zenye mfumo wa kijeshi zinapaswa ziwe na hao wanajeshi, lakini wenye ujuzi na weledi wa uhifadhi. Kuna taarifa kwamba upo mpango wa kuwang’oa watumishi wengine 150 katika moja ya taasisi hizi.
Hii pangua-pangua ya kuondoa watu wenye ujuzi na maarifa ya uhifadhi na kuweka wale wa kukidhi kiu ya wakubwa, inaua uhifadhi. Leo vichwa vingi vya maana katika kwenye nyanja ya uhifadhi vimetupwa taasisi nyingine. Hii ni kasoro.
Mwisho, sote tuwe radhi kulinda rasilimali hii tukitambua kuwa ni wajibu tulionao kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; Ibara ya 27 (1) na (2) inatamka:
27.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”
Nadhani nimetimiza wajibu wangu kwa nia njema, nikiamini si yote ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ataambiwa. Kama hili la OC kwenye hizi taasisi, kwa namna anavyoupenda uhifadhi, akilijua – umma utaona. Hali ya uhifadhi ni mbaya.