Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, aliyekuwa Kidunda

Wiki moja iliyopita, nimepata fursa ya kutembelea ujenzi wa Bwawa la Kidunda, lililopo mkoani Morogoro. Ujenzi wa Bawawa hili umeanza rasmi mwaka 2023 na unatarajia kukamilika mwaka 2026 kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 329. Nimeambiwa fedha hizi zinatokana na vyanzo vya ndani. Ni fedha zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na si za wafadhili.

Sitanii, katika miaka ya 2000 nilikuwa naripoti habari za Bunge. Kwa ukame uliokuwa umelikumba taifa mwaka 1995 na baadaye mwaka 2006, hapo nataja miaka iliyokithiria, ila karibu miaka yote Jiji la Dar es Salaam lilikuwa linapata maji ya mgawo kutokana na ukame unaopunguza maji katika mto Ruvu na hivyo kupunguza uzalishaji wa maji yanayopelekwa Dar es Salaam na Pwani.

Nimerejea miaka ya kuripoti habari za bunge si kwa jambo jingine, bali kila mwaka mawaziri waliosimamia sekta ya maji, walikuwa wanaahidi ujenzi wa Bwawa la Kidunda kama suluhuhisho la mgawo wa maji kwa Jiji la Dar es Salaam na mikoa jirani. Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni kama lita milioni 500 au zaidi kidogo kwa siku ukifanya wastani, lakini wakati wa ukame uzalishaji hufikia mahala ukashuka hadi chini ya lita milioni 100,000.

Kwa takwimu za mwaka 2024 Dar es Salaam na Pwani (Bagamoyo na Kibaha), zilikadiriwa kuwa na mahitaji halisi ya maji wastani wa lita milioni 685.6 kwa siku, lakini uwezo wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka kuzalisha maji ulikuwa ni lita milioni 534.6. Unaweza kufikiria uzalishaji wa maji ya Mto Ruvu unaotoa asilimia 87 ya maji yote unaposhuka uzalishaji kuwa chini ya lita milioni 100 kwa siku wakati wa kiangazi hali inakuwaje.

Sitanii, mawaziri na wabunge aliimba Bawawa la Kidunda, hadi kila Mtanzania akalifahamu kichwani. Sasa nikwambie jambo msomaji wangu. Wakoloni Waingereza miaka ya 1950 walibaini kuwa Mto Ruvu zipo nyakati utakauka kutokana na ukame, hivyo wakati wanajenga chanzo cha maji cha Ruvu Juu, walifanya utafiti na kupendekeza lijengwe Bwawa la Kidunda kwa ajili ya kuhifadhi maji ambayo yatatumika wakati wa kiangazi.

Kuanzia serikali ya Awamu ya Kwanza hadi Awamu ya Tano, bwawa hili lilionekana kwenye mipango ya serikali. Wafadhili waliendewa wakakataa kutoa fedha za kujenga bwawa hili. Mwaka 2021 na 2022, Tanzania ilikumbwa na ukame wa aina yake. Mgawo wa maji ukarejea. Ni kutokana na ukame huu, mwaka 2023 visima vya Kimbiji, ambavyo navyo viliimbwa miaka mingi, Rais Samia Suluhu Hassan akatoa fedha za ndani vikachimbwa.

Kama hiyo haitoshi, Rais Samia akaamua atumie fedha za ndani kujenga Bwawa la Kidunda. Ujenzi umeanza mwaka 2023 na utakamilika mwaka 2026. Bawawa hili litakapokamilika mwakani, litaendelea kutoa maji kwa wastani wa lita bilioni mbili (2) kwa siku kwa mwaka mzima. Hii inamaanisha kuwa Mto Ruvu ambao unazalisha asilimia 87 ya maji yanayotumika Dar es Salaam na Pwani, hautakauka tena.

Ndiyo, mahitaji yanaongezeka, ambapo DAWASA wanakisia kuwa kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, ujenzi wa viwanda na idadi ya watu ifikapo mwaka 2037 mahitaji halisi ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam na mikoa jirani yatakuwa wastani wa lita bilioni 1.2 kwa siku. Idadi ya watu watakaokuwa wanahudumiwa wakati huo inakisiwa kuwa itafikia watu 10,148,287.

Sitanii, bado unaona kama Mto Ruvu utaendelea kutiririsha lita bilioni 2 kwa siku kwa msaada wa Bwawa la Kidunda bila kujali kuwa ni kiangazi au masika, hata mwaka 2037 mitambo ya maji ikipanuliwa mto huu utaendelea kuzalisha maji ya kutosha. Nafahamu kuwa DAWASA wanaendelea na mpango wa kuzalisha maji kutoka Mto Rufiji kutokana na ukuaji wa mahitaji kwani inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2052 idadi ya watumiaji wa maji itafikia 17,867,939 huku mahitaji yakiwa lita bilioni 2.1 kwa siku.

Ninachozungumza hapa ni Bwawa la Kidunda. Mkoloni wakati anajenga mtambo wa Ruvu Juu miaka ya 1950, aliona mbali akabaini umuhimu wa Bwawa la Kidunda kujengwa. Sisi tumekuja kutekeleza mradi huu miaka 64 baada ya Uhuru kwa uamuzi wa Rais Samia. Najiuliza kama Rais Samia ameweza kujenga bwawa hili kwa fedha za ndani, tulikwama wapi miaka yote hii?

Hapa lipo jambo wasilolipenda Watanzania wengi, ila mimi nadhani ni la msingi. Tanzania hii tumeshuhudia viongozi wanne, ambao wamefanya maamuzi magumu na mambo yakaenda. Wa kwanza ni Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania. Mzee huyu alijenga taifa imara lenye umoja, mshikamano na lililoelimika. Sifa za Mwalimu Nyerere ni vigumu kuzifanyia ulinganisho popote.

Mwingine ambaye kila kukicha watu wanatafuta ufutio kufuta nyayo zake, na ingawa hakupata kuwa Rais wa Tanzania, lakini amefanya uamuzi mkubwa na usiofutika ukatelelezwa ni Edward Ngoyai Lowassa. Mwaka 2024 akiwa Waziri wa Maji tu, alifanya uamuzi mgumu kwa niaba ya nchi tukiwa Cairo, Misri ambapo aliwambia Wamisiri kuwa Tanzania ina haki ya kutumia maji ya Ziwa Victoria.

Wamisri walitishia kwenye kikao kuwa Tanzania ikitumia maji ya Ziwa Victoria bila ruhusa yao, wangepigana vita na Tanzania. Lowassa akawambia “Mmechelewa, kama mliitaka hii vita mlipaswa kuanza jana na hata sasa anzeni.” Kauli hii ilimtisha aliyekuwa Waziri wa Rasilimali Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dk. Mahmoud Abu-Zeid aliyewaka, lakini haikufua dafu. Lowassa alimwambia mkataba unayahusu makoloni Uingereza na Tanganyika haikuwahi kuwa koloni la Uingereza. Mchezo uliishia hapo.

Msimamo huo wa Lowassa umewezesha ujenzi wa mradi wa Maji kutoka Mwanza hadi Shinyanga na Kahama. Kwa sasa maji haya yamekwishakwenda Nzega na Tabora, upo mpago wa kuyafikisha Dodoma. Si hayo tu, alijenga mradi wa maji wa Chalinze. Mambo ni mengi aliyofanya, nimegusia kwa uchache hayo mawili. Ni bahati mbaya kuwa hata mwaka mmoja baada ya kifo chake, wapo watu wameshikilia ufutio kufuta historia ya Lowassa isiyofutika.

Sitanii, mtu wa tatu aliyefanya uamuzi usiofutika ni hayati, Rais John Pombe Magufuli. Huyu kwa kuwa mengi ameyafanya karibuni, Watanzania wengi wana kumbukumbu nayo. Nitayataja kwa ufupi. Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere. Ingawa alifariki (Machi 17, 2021) ujenzi wa Bwawa ukiwa katika asilimia 30, ile kuamua kuanza ujenzi tu, ilikuwa ni uamuzi mgumu. Wafadhili walilipinga.

Jambo jingine, Mafufuli akiwa Waziri wa Ujenzi alianzisha mpango wa Build Operate and Transfer (BOT) chini ya Rais Benjamin Mkapa. Nitaje barabara mbili tu, kati ya nyingi alizozijenga. Barabara ya Dar es Salaam – Kibiti – Rufiji – Somanga – Nangurukuru – Mbwemkuru – Lindi – Mingoyo – Mtwara, ikijumuisha ujenzi wa Daraja la Mkapa katika Mto Rufiji hautasahaulika kamwe. Barabara ya Dar es Salaam – Singida – Nzega – Tinde – Kahama – Lusaunga – Biharamulo – Bukoba – Mtukula, haitasahaulika.

Nigusie miradi mingine michache ya Magufuli. Uamuzi wa kujenga treni ya mwendokazi (SGR) japo aliacha haijaanza kufanya kazi Dar – Morogoro, ufufaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na uhamishaji wa makao makuu kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, haya matatu nayo, bila kusahau kuanzisha jenzi wa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki la Busisi/Kigongo, hayafutiki katika historia.

Sitanii, hapo juu nimetaja Bwawa la Kiduna lililoshindikana tangu enzi za mkoloni. Serikali za awamu tano zilizotangulia, zililishindwa. Leo, Rais Samia Suluhu Hassan amepambana linajengwa na mwakani linakamilika. Si bwawa la Kidunda tu, ndiyo maana nimesema watu wanne katika nchi hii. Ukiangalia kiuhalisia mwaka 2021 wakati Rais Samia anachukua nchi, Bwawa la Mwalimu Nyerere ujenzi ulikuwa katika asilimia 30, leo amekamiisha mradi huu mkubwa unaozalisha megawati 2,115 na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye umeme mwingi kuliko nchi yoyote Afrika Mashariki, umekalimika kwa asilimia 99.9.

Haikuwa kazi rahisi kukusanya Sh trilioni 6.5 kukamilisha Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere. SGR kama nilivyotangulia kusema, sote tunafahamu kuwa wakati anafariki Magufuli mwaka 2021 hata kipande cha Dar es Salaam Morogoro kilikuwa hakijakamilika. Rais Samia amevaa ushujaa na kukamilisha si tu kipande cha Dar – Morogoro, bali sasa SGR inafanya kazi kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa sasa.

Rais Samia anaendelea na ujenzi wa SGR kipande cha Dodoma – Tabora – Tabora – Nzega – Isaka – Mwanza na kingine Tabora – Kigoma. Mradi huu kwa ujumla unatumia zaidi ya Sh trilioni 10. Hizi ni fedha nyingi. Kuna wakati nakaa chini najiuliza zinatoka wapi, sipati jibu. Mwanza nako daraja la Kigonga – Busisi katika ziwa Victoria linalounganisha Mwanza na Geita, ambalo wakati Magufuli anafariki lilikuwa hatua za mwanzo kabisa, mwaka huu linazinduliwa.

Sitazungumzia kazi kubwa na ya kupigiwa mfano aliyoifanya Rais Samia kwa kujenga madarasa zaidi ya 30,000 nchini, wala shule za maghorofa na vituo vya afya nchi nzima. Sitazungumzia ujenzi wa barabara za vijijini kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) ambapo babaraba zinachongwa hadi vijijini kwa sasa. Na wala sitazungumzia Tanzania kurejesha heshima yake katika diplomasia na anga za kimataifa ambapo karibu nchi zote duniani kwa sasa zinatamani kufanya kazi na Tanzania chini ya Rais Samia.

Sitanii, nimeyasema yote haya kutokana kazi ya kihistoria aliyofanya Rais Samia kujenga Bwawa la Kidunda. Nafahamu yapo mengi ameyatenda na anaendelea kutenda. Jambo moja linalonijia kichwani, najiuliza. Hivi Rais Samia akimaliza miradi hii mikubwa kwa asilimia 100 kama nchi tunakwenda likizo au tunaanzisha miradi mingine?

Jibu linalonijia kichwani ni tusilale. Kama ambavyo leo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) alivyofikisha umeme vijiji vyote vya Tanzania na sasa tunakwenda kwenye vitongoji, basi Rais Samia anapotua mzigo wa malipo makubwa ya Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bwawa la Kidunda, Daraja la Magufuli, Shirika la Ndege (ATCL), SGR na mingine, sasa tuanze utekelezaji wa miradi mingine mikubwa ikiwamo mradi wa gesi asilia (LNG) Lindi, tujenge mabomba ya gesi kwenda nchi jirani tuuze gesi na mingine.

Lakini pia ukiniuliza, nasema tuanze kutandika SGR kutoka Dodoma kwenda Arusha kilomita 430, Dodoma – Iringa kilomita 290, ambako itaungana na TAZARA iliyoboreshwa, kisha tuwaze kutandika SGR – Ruvu – Chalinze – Segera – Tanga – Kilimanjaro – Arusha. Nafahamu ni kazi kubwa, ila tukiweza muunganiko huu, uchumi utakua kwa kasi ya China.

Sitanii, nihitimishe kwa kumpa pongezi Rais Samia kwa uamuzi huu wa kihistoria juu ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda na DAWASA wanaousimamia, mradi huu ambao unakwenda kumaliza kabisa tatizo la maji jijini Dar es Salaam. Ukiniuliza nchi yetu inaelekea wapi chini ya Rais Samia, nitakwambia; yajayo yanafurahisha. Tukutane wiki ijayo. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827