Baada ya Sudan kutangaza nia ya kuchukua hatua kali dhidi ya Kenya kwa kile ilichokiita kuunga mkono wanamgambo wa RSF kwa kuwapa nafasi ya kufanya mkutano jijini Nairobi, Kenya imejitokeza kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Nje, Kenya imeeleza kuwa haijavunja sheria zozote za kimataifa, ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa, misingi ya Umoja wa Afrika, wala Mkataba wa Kuzuia Uhalifu wa Kimbari.

Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa kuwapo kwa RSF jijini Nairobi ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kutafuta amani, ikizingatiwa kuwa mara nyingi pande zinazozozana huandaa mazungumzo katika nchi nyingine zisizo sehemu ya mgogoro.

“Kenya inaunga mkono suluhu za amani na inatoa nafasi kwa mazungumzo yanayolenga kumaliza mizozo ya kisiasa bila kupendelea upande wowote,” ilisema taarifa hiyo.

Licha ya lawama kutoka kwa Sudan, Kenya imeeleza kuwa lengo lake ni kutoa mazingira salama kwa makundi yanayohusika katika mgogoro wa Sudan, yakiwemo RSF na mashirika ya kiraia, ili kutafuta njia za kurejesha utawala wa kiraia nchini humo.

“Tuna matumaini kuwa watu wa Sudan wataweza kufikia makubaliano yatakayosaidia kurejesha utulivu,” imeeleza serikali ya Kenya.

Mbali na hilo, Kenya imetangaza msaada wa dola milioni 2 ili kusaidia juhudi za kibinadamu zinazolenga kupunguza mateso ya wananchi wa Sudan wanaoathirika na mgogoro huo.

Katika hatua nyingine, RSF imetangaza kuwa itatoa tamko rasmi kwa vyombo vya habari leo, huku taarifa zikieleza kuwa wanamgambo hao wanatarajia kusaini makubaliano ya kuunda serikali mbadala ndani ya Sudan, mchakato ambao utafanyika Nairobi siku ya Ijumaa.

Kenya, ikiwa na historia ya kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani, imekumbusha kuwa mwaka 2002 ilisaidia kufanikisha Mkataba wa Machakos uliomaliza vita vya muda mrefu vya Sudan. Serikali imeendelea kusisitiza kuwa njia za kidiplomasia ndizo zenye ufanisi zaidi katika kusuluhisha migogoro ya kisiasa badala ya mapambano ya kijeshi.