Mwanasiasa maarufu wa Uganda Dk Kizza Besigye amefikishwa katika Mahakama Kuu mjini Kampala kusikiliza ombi la mawakili wake la kumtaka achiliwe huru.

Besigye ambaye amesusia chakula tangu wiki iliopita alionekana kudhoofika huku akiandamana na mshtakiwa mwenzake Haji Obeid Lutale.

Awali jaji wa Mahakama Kuu aliaamrisha waandishi habari kuondoka nje ya kikao cha mahakama na baada ya kufanya mkutano wa faragha na upande unaomtetea Besigye, waandishi habari walirejea kwenye kikao hicho.

Douglas Singiza, Jaji wa Mahakam Kuu ya Uganda ameagiza maafisa wa gereza kuwarejesha Besigye na Lutale gerezani, kutokana na kudhoofika kwa afya yake.

Kwa sasa kikao cha Mahakama kinaendelea bila wawili hao. Mawakili wanaitaka Besigye aachiliwa kwa misingi ya matibabu.

Jaji huyo ameagiza Besigye na mshtakiwa mwenzake kurejeshwa gerezani. Jana Waziri wa sheria na masuala ya Kikatiba Nobert Mao aliliambia bunge kuwa Mahakama kuu ya Uganda itaanza mchakato wa kusikiliza ombi la mawakili wa Mwanasiasa huyo ungeanza leo, badala ya Juma nne ya wiki ijayo kama ilivyokuwa imepangawa awali.

Wakili wa Besigye Eron Kiiza ambaye awali alihstakiwa na kuhukumiwa miezi tisa jela na mahakama ya kijeshi, pia amefikishwa mahakamani.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni kupitia mtandao wake wa X jana alishtumu Mahakama kuu zaidi nchini humo kwa kuchelewesha mchakato wa kesi ya mwanasiasa huyo wa upinzani ilipotoa uamuzi wa kuivua mamlaka ya kisheria Mahakama ya kijeshi kusikiliza kesi za raia wa kawaida.