Rais wa Marekani, Donald Trump, ameikosoa Ukraine kufuatia kauli ya Rais Volodymyr Zelensky, aliyeeleza kushangazwa na kutohusishwa kwa nchi yake katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika Saudi Arabia.

Mazungumzo hayo yalilenga kutafuta suluhisho la kumaliza vita vya Ukraine vilivyoanza karibu miaka mitatu iliyopita baada ya Urusi kuivamia nchi hiyo.

Trump alieleza kukasirishwa na msimamo wa Ukraine, akidai kuwa nchi hiyo ingeweza kufikia makubaliano ya kumaliza vita mapema.

Kauli yake ilijiri baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, kusema kuwa Urusi haitakubali majeshi ya NATO kupelekwa Ukraine kama sehemu ya mkataba wowote wa amani. Haya yalizungumzwa baada ya Lavrov kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, nchini Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa taarifa za pande zote, Urusi na Marekani zimekubaliana kuunda timu zitakazoshughulikia mazungumzo ya kusitisha vita.

Trump, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Mar-a-Lago, alijibu swali la BBC kuhusu hisia za Ukraine juu ya kutengwa kwenye mazungumzo.

Alisema, “Nasikia wameudhika kwa kutoshirikishwa, ingawa wamekuwa na nafasi hiyo kwa miaka mitatu na hata kabla ya hapo.”

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa mataifa ya Ulaya kutuma wanajeshi Ukraine, Trump alijibu, “Iwapo wanataka kufanya hivyo, ni sawa kabisa, niko tayari kuhusu hilo.”