Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya amekipongeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuendesha uchaguzi wa ndani kwa uwazi na kufuata misingi ya demokrasia.

Pongezi hizo amezitoa leo Februari 13, 2025 bungeni jijini Dodoma, wakati wa mjadala wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambapo amemtaja Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kama kiongozi aliyeonyesha uwezo mkubwa wa kuiongoza Chadema kuelekea demokrasia ya kweli.

“Kwa moyo wa dhati, naipoingeza Chadema kwa kuonesha mfano wa uchaguzi huru na haki. Pia nampongeza Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kukubali matokeo na kuweka mbele maslahi ya demokrasia,” amesema Bulaya.

Amesema Lissu ana uzoefu mkubwa wa uongozi ndani ya Chadema, aliwahi kushika nafasi mbalimbali, ikiwemo ya Makamu Mwenyekiti, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.

“Historia yake inaonyesha kuwa ana sifa na uwezo wa kuongoza chama na kutufikisha kwenye demokrasia ya kweli,” ameongeza Bulaya.