Asema Serikali inajivunia uwepo wa viwanda vya kuongeza thamani madini nchini
π Dodoma,
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa, Serikali ya Tanzania inatambua kuwa ili kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) kifanye kazi kwa ufanisi, kinahitaji upatikanaji wa dhahabu ya kutosha (feed stock) na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati ya kufanikisha jambo hilo.
Aliyasema hayo, Februari 11, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza katika semina iliyoandaliwa kwa ajili ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494311-1024x692.jpg)
Mhe. Mavunde alibainisha kuwa Serikali imeshafanya kikao cha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wadau wote muhimu ili kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa mitaji kwa Watanzania kupitia mpango wa Export Credit Guarantee Scheme.
Aidha, Waziri Mavunde alisema kuwa, Serikali inaendelea na juhudi za kuhamasisha wachimbaji wadogo kuanza kuuza dhahabu yao katika viwanda vya ndani ikiwemo GGR, jambo ambalo litawanufaisha kwa kupata bei nzuri, kupunguza gharama za usafirishaji, na kufurahia punguzo la tozo zilizowekwa kwa dhahabu inayosafishwa ndani ya nchi.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494312-1024x708.jpg)
Dhamira ya Serikali katika Uongezaji Thamani wa Madini
Mhe. Mavunde alieleza kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa madini yanayochimbwa hapa nchini yanaongezewa thamani hapahapa nchini, hatua inayolenga kuongeza mapato ya Serikali, kutoa ajira kwa Watanzania, na kusaidia sekta nyingine zinazohusiana na madini, kama vile benki na viwanda vya vifaa vya uchimbaji kuendelea kupata masoko.
Alisisitiza kuwa, GGR ni kiwanda cha kisasa chenye hadhi ya kimataifa ambacho kimekuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya madini nchini. βTuna furaha kuona kwamba sasa Tanzania inayo miundombinu ya hali ya juu kwa ajili ya usafishaji wa dhahabu, jambo ambalo linaipa nchi yetu hadhi kubwa katika soko la madini duniani,β amesema Mavunde.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494313-1024x730.jpg)
Serikali yajivunia uwepo wa GGR
Waziri Mavunde alieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge kuwa, Serikali ya Tanzania inajivunia uwepo wa viwanda vya uongezaji thamani madini hapa nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa kiwango cha juu zaidi na kwamba mojawapo ya mafanikio makubwa katika Sekta ya Madini ni uwepo wa Kiwanda cha kisasa cha kusafisha madini ya dhahabu, Geita Gold Refinery (GGR), kilichopo mkoani Geita.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa alisisitiza kuwa, licha ya dhamira njema ya Serikali kulinda viwanda vya ndani vya uongezaji thamani madini, ipo haja ya vitengo vya masoko vya viwanda husika kufanya utafiti kuhusu mbinu zingine za kimasoko kutokana na ushindani wa kibiashara ili kupata malighafi nyingi zaidi bila kuvunja maadili yanayotakiwa kwa kuzingatia kuwa viwanda hivyo vina hadhi ya kimataifa.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494319-1024x682.jpg)
Mazingira Rafiki ya Kibiashara kwa Wachimbaji wa Dhahabu
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba alifafanua kuwa, ili kusaidia upatikanaji wa kutosha wa Malighafi (Feed Stock) kwa GGR, Serikali imeweka mazingira bora ya kibiashara kwa wachimbaji wa dhahabu, ikiwa ni pamoja na kupunguza jumla ya tozo kwa dhahabu inayosafishwa katika viwanda vya ndani ikiwemo GGR, tozo zimepungua hadi asilimia 6.3, ikilinganishwa na asilimia 9.3 zinazotozwa katika masoko mengine.
Mhandisi Samamba aliongeza kuwa, hatua hiyo imelenga kuwahamasisha wachimbaji wadogo na wa kati kuuza dhahabu yao katika viwanda vya ndani kama GGR badala ya kuuza katika masoko mengine ikiwa bado haijasafishwa kwa kiwango cha kimataifa.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494324-1024x703.jpg)
Bunge Lapongeza Uwekezaji wa GGR
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. Mathayo David kwa niaba ya kamati hiyo, alimpongeza Bi. Mwanahamisi Masasi, maarufu kama Mama Masasi mmoja wa wawekezaji wakubwa katika mradi wa Geita Gold Refinery, kwa uthubutu na hatua kubwa alizopiga katika kuanzisha na kuendeleza kiwanda hicho.
Dkt. Mathayo alieleza kuwa, uwekezaji huo ni wa kihistoria na una manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi, hususan katika sekta ya madini huku akiitaka Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa aina hiyo katika madini mengine pia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zake za madini.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494325-1024x681.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494326-1024x702.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494322-1024x682.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494323-1024x682.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494327-1024x690.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494328-1024x682.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002494329-1024x682.jpg)