Na Aziza Nangwa ,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Walaji wa nyama ya ng’ombe na wananchi kwa ujumla wameonywa kuhusu kuwapo kwa wafanyabiashara wanaolihujumu soko la nyama hiyo inayotumiwa kwa wingi nchini.

Hujuma hizo hufanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanaonenepesha ng’ombe kinyume cha taratibu stahiki.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wataalamu wa mifugo ambaye ni daktari wa mifugo, Dk. Theoduli Laurence, amesema unenepeshaji kwa kuwadunga ng’ombe dozi kubwa ya aina fulani ya dawa si sahihi.

“Kuna wafugaji wasio waaminifu ambao huwadunga ng’ombe dozi kubwa ya ‘Ivermectin Injectable’ na ‘parasiticide for cattle – solution’. Hizi si za kunenepesha, ni matumizi mabaya ya dawa. Wanawachoma wanyama kuwanenepesha ili wapate pesa nyingi sokoni.

“Kwa ng’ombe kudungwa dawa na kuchinjwa kabla ya muda, ni hatari kwa afya ya binadamu. Kunaweza kusababisha magonjwa ya figo, moyo, maini na mengine sugu baada ya miaka michache tu ya kula nyama au maziwa,” amesema.

Kwa mantiki hiyo, wataalamu wanaweka wazi kuwa ni bora kula kuku wa kisasa kuliko nyama ya ng’ombe walionenepeshwa kwa njia isiyo sahihi.

Utafiti uliofanywa na wataalamu hao umebaini kuwa nyama nyingi zinazouzwa sasa zimepoteza harufu yake ya asili kutokana na matumizi holela ya dawa za kunenepesha.

Chanzo kikubwa cha haya, kwa mujibu wa uchunguzi wa JAMHURI, ni tamaa ya fedha kwa wafugaji ambao sasa hawajali tena afya ya mlaji.

Mbali na nyama kupoteza harufu yake ya asili hata ikichomwa, pia ladha nayo imepotea.

Dk. Laurence amesema ni vema kuchukua hatua pindi utakaposhindwa kuielewa nyama iliyopo buchani.

“Kitaalamu, dawa hizi hutakiwa ng’ombe adungwe kulingana na uzito wake. Kuna kiwango rasmi cha matumizi ili mifugo iwe salama kwa mfugaji na walaji baada ya kuchinjwa. Mfano, ng’ombe mwenye uzito wa kilo 100, anatakiwa kupigwa ‘pisi mbili’ tu, si zaidi,” amesema.

Amesema kwa sasa wafugaji huwadunga ng’ombe kati ya ‘pisi’ 10 hadi 20 ili wanenepe haraka na kuwauza kwa faida.

“Sasa mtu unaponunua aina hii ya ng’ombe, unakuwa haujanunua nyama ila umenunua sumu mbaya kwa mwili wako. Dawa hizi ni za kutibu mifugo na hutumiwa kwa uangalifu kwenye kuondoa vipele kwenye ngozi na minyoo,” amesema.

Amesema baada ya dawa hizo kutumiwa na ng’ombe kunenepa, mnyama huyo hapaswi kuuzwa kwa ajili ya kuchinjwa wala maziwa yake kutumika hadi baada ya siku 28.

Hali ilivyo mijini

JAMHURI limeelezwa kuwa kwa sasa tatizo la nyama zenye sumu ni kubwa na baya zaidi kuliko hata tatizo la uuzaji wa sumu za panya, mende, kunguni na wadudu wengine.

“Kwa kula nyama yenye sumu hizi kunaweza kusababisha kuharibika kwa seli, hivyo kusababisha ongezeko la magonjwa kama kansa ya ini, kansa ya utumbo na kufeli kwa figo,” amesema mtaalamu mwingine na kuongeza:

“Watu wengi wanaojitambua hawali tena nyama kwani ni hatari sana. Hapa hata kuku wa kisasa pamoja na changamoto zao, katika hili wanasubiri.”

Pamoja na elimu kutolewa, bado viuatilifu na dawa za mifugo ni kama havina usimamizi mzuri, na wafugaji wanajali zaidi masilahi yao binafsi.

Wataalamu wanadai kwamba sumu yoyote ni hatari hata kama inaua mdudu mdogo. Ndiyo maana kila dawa huambatana na tahadhari ya kuwekwa mbali na watoto, kwani masharti yasipozingatiwa athari ni kwa jamii.

“Kwa sasa ni Mungu tu ndiye anayetulinda, ndiyo maana bado tunaendelea kuishi. Njia ya kujikinga kama jamii ni kuzuia madhara yasitokee, kwa kutoa elimu kwa jamii na kuweka udhibiti wa uuzaji. Tunaweza kufikia udhibiti wa asilimia 60 hadi 70,” amesema.

Dk. Winston Bill, Mkaguzi kutoka Wizara ya Mifugo, anasema ng’ombe kudungwa dawa bila kufuata ushauri wa daktari ni kosa, na ni hatari kwa maisha ya binadamu.

“Kisheria kumchoma ng’ombe dozi kubwa ili kuwafanya wanenepe ni kosa, ingawa sijaliona hili moja kwa moja, najua kuwa watu wanajihusisha na vitendo hivi na tumekuwa tukipiga kelele sana na kutoa elimu kwa wafugaji.

“Kilichopo kwa sasa wafanyabiashara wanataka kutumia mwanya wa biashara ni huria kutuangamiza, kwa sababu wanapaswa kuzingatia afya za wanyama wao na wenzao,” amesema.

Dk. Bill anasisitiza kuwa matibabu ya wanyama yanapaswa kufanywa na wataalamu.

“Changamoto iliyopo wafugaji wengi wanajiona kama wataalamu, wanachoma wanyama bila kufuata taratibu na hii ni hatari kwa afya zetu. Wananunua dawa na kuzipeleka mashambani bila usimamizi wa kitaalamu, wanafanya watakavyo ili kupata faida,” amesema.

Amesema hali hii inasababisha matatizo kwa jamii, kwani mfugaji akishindwa kufuata utaratibu anaweza kumchinja ng’ombe kabla hata siku 28 hazijapita ili dawa iishe kwenye mwili wa mnyama.

“Mikakati yetu kama wakaguzi ni kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji ili kukabiliana na changamoto hizi. Aidha, tunatarajia kudhibiti uuzaji wa dawa za mifugo minadani,” amesema.

Anawashauri wafugaji kuacha mara moja vitendo vya aina hii, kwani madhara yake ni makubwa na yanaweza kujitokeza hata baada ya miaka minne au zaidi.

Amesema si rahisi kuitambua nyama yenye sumu kwa macho, bali ni kwa kutumia vipimo maalumu vya maabara na utaalamu.

Kauli za wataalamu zinaungwa mkono na daktari mwingine wa mifugo, Dk. Jeremia Njile, akisema ng’ombe hunenepa baada ya kudungwa dawa, kwa sababu wadudu wa maradhi kama minyoo huondoka mwilini mwake.

“Ikiwa atachomwa zaidi ya kiwango, kuna hatari ya mnyama kupoteza maisha au kunenepa kupita kiasi.

“Pia kama dozi kubwa atapatiwa mnyama kama paka au mbwa,  anaweza kupata ugonjwa wa kupepesuka kwa siku tatu au nne,” amesema.

Kuhusu kutambua uwepo wa sumu kwenye nyama, Dk. Njile anasema ni lazima kupimwa maabara.

Anasema mtu wa kawaida anaweza tu kuangalia kwa macho na  kuona alama ya sindano kwenye sehemu ya nyama ya ng’ombe kwani huwa haijifichi, huku pia ini likiwa na rangi ya njano.

“Kwa sasa ninachokiona ni  changamoto ya uelewa kwa baadhi ya wafugaji, ambao mara nyingi hawajui madhara ya matumizi ya dawa hizi, na wanaweza kufanya hivyo kwa faida zao binafsi bila kujua hatari zinazoweza kuja,” amesema.