Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamsaka Abdallah Mohammed (40), fundi friji na mkazi wa Mataya, Kata ya Kiromo, Wilaya ya Bagamoyo, kwa tuhuma za mauaji ya mzazi mwenzake Naomi Mwakajengele ( Anangisye) miaka 28, mwalimu wa Shule ya Msingi Mataya.

Uchunguzi wa awali unaonyesha mwili wa marehemu Naomi umechomwa na kitu chenye ncha kali kwenye maeneo ya ubavu wa kulia, ubavu wa kushoto, na kwenye chembe ya moyo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Salim Morcase alieleza kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia februari 11, ambapo wawili hao walikuwa chumbani kwao ambapo kelele za kilio cha Naomi, akidai kuwa mwenza wake anamuua, zilisikika kutoka kwenye chumba chao.

Anasema, baada ya kelele hizo, Abdallah Mohammed alitoka chumbani na akaenda kwa dada wa kazi na kumtaka kulala na watoto wao wawili, mwenye umri wa miaka 4 na mwingine wa miaka 2, ambao awali walikuwa wamelala na mama yao.

Morcase anafafanua,asubuhi, dada wa kazi alishtuka baada ya kuona mlango wa nyumba ukiwa wazi na Abdallah Mohammed akiwa ametoweka, bila kujua alipoenda.

“Inavyoonekana, wawili hao walikuwa na migogoro ya muda mrefu, hali iliyopelekea kutokuishi pamoja kwa kipindi fulani kabla ya Abdallah kurejea tena nyumbani kwa Naomi wiki mbili zilizopita, hatimaye, tukio hilo lilitokea.

Morcase, alitoa wito kwa yeyote atakayemuona Abdallah Mohammed au kuwa na taarifa zozote kuhusu alipo, kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali, au chombo chochote cha dola ili aweze kukamatwa na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.