Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mwenyeji wa mkutano huu, umeongozwa na wenyeviti wawili; William Ruto wa Kenya, ambaye ni Mwenyekiti wa EAC na Emmerson Mnangagwa, ambaye ni Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa SADC.

Sitanii, mkutano huu umehudhuriwa na marais tisa na viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama. Nchi mbili zinazogombana; Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zimehudhuria ila Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amekuwapo ukumbini Ikulu na Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, alihudhuria kwa njia ya mtandao.

Wapo waliohoji kwa nini Tshisekedi alihudhuria kwa njia ya mtandao. Nadhani wamesahau yaliyomkuta aliyekuwa Rais wa Bundi, Pierre Nkurunziza, Mei 13, 2015.

Siku hiyo hayati Nkurunziza akiwa kwenye kikao cha usuluhishi na waasi, Meja Jenerali Godefroid Niyombareh, alitangaza kumpindua.

Joto lilikuwa juu nchini humo, hali iliyowafanya polisi kutoka mitaani wakawaacha wananchi wanashangilia barabarani. Hata hivyo, kwa umahiri na ustadi wa pekee, Nkurunziza alirejea Bujumbura na Niyombareh akatokomea kusikojulikana. Si ajabu Tshisekedi ameuruka mtego huo.

Sitanii, mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unachangiwa na sababu za kihistoria, kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Koloni la Ubelgiji lilijenga msingi wa unyonyaji wa rasilimali bila kujali maendeleo ya kijamii na miundombinu. Baada ya uhuru mwaka 1960, migogoro ya kisiasa, mapinduzi na utawala wa Mobutu Sese Seko ulisababisha udhaifu wa taasisi za serikali.

Vita ya kikanda (1996 – 2003) ilihusisha mataifa jirani kama Rwanda, Uganda na Burundi ambayo yalihusika kwenye uporaji wa rasilimali za DRC kama dhahabu, almasi na coltan.

Migogoro ya kikabila na makundi ya waasi kama M23 pia imeongeza hali ya ukosefu wa usalama. Uingiliaji wa majeshi ya kigeni, usimamizi mbovu wa rasilimali na ukosefu wa maendeleo ya kijamii vimeimarisha mgogoro huu.

Rwanda imetuhumiwa waziwazi kuwa inaunga mkono waasi wa M23. Kundi hili lenye askari jamii ya Banyamulenge, ambao ni Watusi wa Rwanda, ndilo linaloleta shida kubwa nchini humo.

Makundi ya waasi ni mengi nchini DRC. Ukiacha M23, wapo Allied Democratic Forces (ADF), Mai-Mai, Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), Lord’s Resistance Army (LRA) linalotaka kuipindua Serikali ya Uganda.

Si hayo tu, wapo National Liberation Front (FNL), Patriotic Resistance Front of Ituri (FRPI), Bakata Katanga, CODECO (Cooperative for Development of the Congo), Raia Mutomboki, Nyatura, Allied Democratic Forces-Mwalika (ADF-Mwalika), Forces for Patriotic Resistance of Ituri (FPRI), Islamic State Central Africa Province (ISCAP), Simba Militia, Mouvement National Congolais-Lumumba (MNC-L), Union of Congolese Patriots (UPC) na mengine.

Sitanii, unaweza kujiuliza hivi ni kweli makundi haya yanapigania uhuru wa wananchi wa DRC? Jibu ni hapana. Marekani imetangaza nia ya kuiwekea vikwazo Rwanda kwani pamoja na kutokuwa na mgodi wa dhahabu mwaka jana imeuza dhababu yenye thamani ya dola bilioni 1.1. Waasi wa M23 inaowaunga mkono wametega mgodi wa Coltan unaozalisha madini hayo kwa wingi, ila yanauzwa kwa njia za panya.

Sitanii, nimesoma tamko la pamoja la wakuu wa nchi za EAC na SADC. Kimsingi naona kama wameipapasa Rwanda. Rwanda kumwambia andoe majeshi ambayo hayajaalikwa bila kumshurutisha, ilhali anapata mabilioni ya dola kwa uwepo wa M23, ni jambo lisilowezekana.

Labda, nasema, kwa kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameonyesha mwelekeo wa kutopenda vita na kusitishwa kwa misaada ya Marekani iliyokuwa inatolewa hata kwa vikundi vya waasi duniani, huenda likafanikiwa. Ila, ifahamike kuwa Wazungu ndio wanaochimba na kufaidi madini ya DRC kupitia mawakala wao.

EAC/SADC wanapendekeza njia ya Diplomasia na Mazungumzo. Wanasema juhudi zifanywe kuimarisha mazungumzo kati ya makundi hasimu, Serikali ya DRC na nchi jirani (Rwanda na Uganda) kutatua chanzo cha migogoro ya kikabila na kisiasa.

Wataalamu wanapendekeza usimamizi wa rasilimali. Wanataka kuziwajibisha kampuni za kimataifa zinazochimba madini DRC na kudhibiti rasilimali asilia kwa njia inayofaidisha wananchi wa DRC.

Pendekezo jingine ni kuimarisha taasisi za serikali. Jeshi la DRC linaelezwa halijapikwa vizuri. Inahitajika kujenga serikali yenye uwezo wa kudhibiti mipaka, kutoa huduma za msingi na kupambana na ufisadi.

Usaidizi wa jumuiya ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na mashirika mengine kutoa msaada wa kibinadamu na kijeshi kupitia MONUSCO na programu za maendeleo, inaelezwa kuwa itasaidia.

Sitanii, mataifa jirani na DRC yanapaswa kuheshimu mipaka na kujitolea kushirikiana katika kuhakikisha usalama wa kikanda bila kuingilia mambo ya ndani ya DRC.

Kuitoa nchi hii ilipo sasa inapaswa kuwekeza kwenye miradi ya elimu, afya na miundombinu ili kupunguza umaskini na ukosefu wa ajira, ambao huchochea migogoro. Suluhisho la kudumu linahitaji mshikamano wa kitaifa na kimataifa kwa kupambana na mizizi ya mgogoro na kujenga misingi ya amani na maendeleo.

Yote haya yanaweza kufanyika, ila nchi jirani kama Rwanda na Uganda zisipoondoa hofu na tamaa ya kupata mali isiyo halali, mgogoro wa DRC itakuwa vigumu kumalizika.

Lakini pia, nchi hizi zinapaswa kufahamu kuwa wakubwa hawa wanayo tabia ya kutumia nchi changa kwa muda na wakimaliza hitajio lao watazitelekeza.

Wakumbuke Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa za Banga wa Zaire, alivyotumiwa kisha akaachiwa jangwani. Mungu ibariki Afrika, Mungu tujalie amani.

0784 404827