Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na jitihada za kuongeza na kuwajengea uwezo watumishi wake wakiwemo wachunguzi na waendesha mashitaka ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na kuendeleza maliasili nchini kwa faida ya kizazi cha sasa na kinachokuja.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi Wizara ya Maliasili na Utalii SACC Fidelis Kapalata kwenye ufunguzi wa mafunzo ya uchunguzi wa kifedha kwa watumishi wa wizara ikijumuisha Taasisi za Jeshi la Uhifadhi wanaohudhumu katika vitengo vya upelelezi na uendeshaji mashtaka.

SACC. Kapalata amesema kuwa kutokana na umuhimu wa wanyamapori kwa uchumi wa nchi kupitia utalii, Tanzania imetenga takriban asilimia 32.5 ya eneo lake kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, ambapo utalii unachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni, hivyo ni lazima ulizi imara uwepo ili kuzilinda Maliasili hizo athimu.

“Pamoja na umuhimu wa wanyamapori, mazao ya misitu na nyuki na mchango wa utalii, Wizara imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ujangili wa nyara, biashara haramu ya mazao ya misitu na wanyamapori na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuzitaja kwa uchache tu”. Aliongeza SACC. Kapalata

Aidha SACC. Kapalata amefafanua kuwa, moja ya jitihada zinazofanywa na Wizara katika kulinda Maliasili ni pamoja na kushirikiana na taasisi za Jeshi la Uhifadhi kuandaa Mpango kazi wa utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Maangamizi wa mwaka 2022/23 – 2026/27.

“Napenda kuchukua wasaa huu kuwasihi kuendelea kupambana na utakatishaji fedha haramu hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za Jeshi la Uhifadhi na taasisi zingine vikwemo vyombo vya ulinzi na usalama” Alisisitiza SACC. Kapalata

Sheria iliyoanzisha Jeshi la Uhifadhi imewapa maafisa na askari nguvu mbalimbali ikiwemo kupepeleza, kuendesha mashataka na kuchunguza makosa yote yanayohusiana na wanyamapori na misitu.