Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,Deus Sangu amesema baadhi ya mamlaka za nidhamu hazizingatii sheria ,kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika ushughulikiaji mashauri ya kinidhamu na jambo hilo limeisababishia hasara kubwa Serikali.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024 rufani za watumishi zilizopelekwa Tume ya Utumishi wa Umma na ambazo zilirejeshwa kwa waajiri kutokana na dosari mbalimbali kwa ajili ya kuanza upya zilifikia 275 sawa na asilimia 25.
Naibu Waziri Sangu amesema hayo mjini Morogoro katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi kuhusu mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kieletroniki wa kushughulikia rufaa na malalamiko na Ukaguzi wa Usimamzi wa Masuala ya Rasilimali Watu (PSCMIS) yaliyoandaliwa na tume hiyo.
Mafunzo hayo katika kundi la kwanza yaliwashirikisha maofisa utumishi wa wizara zote, idara zinazojitegemea zilizopo chini ya serikali, pamoja na maofisa Tehama.
“ Maana yake ni nini , ni kwamba tunaisababishia serikali hasara katika maeneo mbalimbali ikizingatiwa uendeshaji wa mashauri ni gharama ikiwemo ya kuunda tume mbalimbali , kamati mbalimbali na vikao vya kwenda kushughulikia mashauri haya,” amesema Sangu.
Naibu Waziri amesema kuwa imebainika kuwa baadhi ya viongozi kwenye taasisi za Umma wamekuwa wakifanya maamuzi kwa hisia , kwa sababu mtumishi fulani hawamtaki ofisini na kwa kuwa wameamua hivyo ni lazima aondoke.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-35-1024x827.png)
“ Wanaanza kushughulikia suala la shauri la nidhamu kwa hisia na bila ya kufuata zile taratibu za kuendesha mashauri ya kinidhamu,” amesema Naibu Waziri Sangu.
Naibu waziri amesema kama hatua ya awali shauri la kinidhamu haikufanyika vyema na yakirudishwa upya mchakato unaanza upya na wakati mwingine mtumishi huyo tayari ameshaondolewa kwenye orodha ya utumishi wa umma.
“ Ikifikia hatua hii unazalisha limbikizo la mshahara na Serikali inaanza kuvuruga bajeti yake kuanza kupanga bajeti ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi ambao wamerejeshwa kazini,”amesema Sangu.
Naibu Waziri ametoa maelekezo mahususi kwa tume hiyo kuhakikisha jukumu lake la kufanya ukaguzi kwenye maeneo ya rasilimali watu kwa watumishi wa umma likatekelezwa .
Hivyo aliitaka inapokwenda kufanya ukaguzi aliangalie kwa uangalifu ili kujua tatizo lipo kwa ukubwa gani ili kupunguza rufaa zinazorudishwa ili kudhibiti mashauri ambayo yanaamuliwa kinyume na sheria, taratibu na kanuni kwa ajili ya kuokoa fedha za serikali isipate hasara .
“ Tunataka tuone kama rufaa zinarudi ni chache ambazo zina sababu za msingi ambazo kweli zikikuwa nje ya uwezo wa wale wanaozisimamia katika mashauri haya ya nidhamu katika hatua ya awali,” amesisitiza Naibu Waziri Sangu.
Naibu Waziri amesema katika eneo hilo ,serikali inapenda kuona uboreshaji wa hali ya juu na katika mwaka huu wa fedha ( 2024/2025) ukaguzi inaendelea kufanyika .
Mbali na hayo alisema Serikali itaendelea kutoa bajeti ya kutosha kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza majukumu yake ya ukaguzi .