Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na maji (EWURA), imekabidhi vifaa vya umwagiliaji maji ikiwemo tenki lenye ujazo wa lita 5000,mabomba, mipira pamoja na vifaa vitakavyotumika kufunga vifaa hivyo vyote vikiwa na thamani ya sh. Milioni mbili kwa kikundi cha umwagiliaji kilichopo Manispaa ya Songea .
Akikabidhi vifaa hivyo jana kwa wanakikundi hao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Songea ,kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA,meneja wa Ewura wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Karim Ally alisema kuwa EWURA wamekabidhi vifaa hivyo ili kuwawezesha vijana wajasiliamali wa mjini Songea viwasaidie katika shughuli za uzalishaji wa kahawa na mbogamboga kwa lengo la kuwaongezea tija ,kupanua ajira na kupunguza umaskini.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002488107.jpg)
” EWURA inajukumu la kuleta matokeo chanya katika kukuza na kuendeleza usatwi wa jamii kwa ujumla nchini Tanzania ili iweze kufikia lengo hili imekuwa ikitenga bajeti ya kuwezesha kuchangia na kutoa msaada mbalimbali kwa jamii kwa mujibu wa sera yetu ya michango na misaada ya mwaka 2021″ alisema Ally.
Alisema kuwa EWURA pia inajukumu la kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji hivyo basi uwekaji wa miundombinu sahihi kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao yao utasaidia katika utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla na si vinginevyo.
Akipokea vifaa hivyo,Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile ameishukuru EWURA kwa namna walivyojitoa kuwasaidia kikundi cha wajasiliamali wangeweza wasiwasaidie kwa sababu msaada ni msaada tu sio lazima wapewe wakiomba.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002488108.jpg)
Aidha amewataka vijana wa Songea kujikita kwenye kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji ambacho kinalipa kwa sababu Mji wa Songea unakuwa kwa kasi na kipindi cha kiangazi utahitaji mkubwa wa mboga mboga na matunda mbalimbali ili kuleta tija.
Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho Benedict Mbawala amewashukuru Ewura kwa kuwasaidia lakini pia Mkuu wa Wilaya ya Songea kwa kuwapambania kupata hivyo vifaa ambavyo vitawasaidia msimu wa kiangazi kwa ajili ya umwagiliaji.