Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo amefika mbele ya mahakama mjini Tel Aviv kujibu mashtaka ya muda mrefu ya rushwa.

Netanyahu aliwasili na timu yake ya mawakili inayoongozwa na Amit Hadad baada ya kuamriwa kutoa ushahidi katika mashtaka ya mwaka 2019 ya kesi tatu zinazohusisha zawadi kutoka kwa marafiki mamilionea pamoja na madai ya kutafuta hisani kutoka kwa maatajiri wa vyombo vya habari kwa kubadilishana na fursa bora ya utangazaji.

Netanyahu amekana mashtaka yote. Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75, ndiye waziri mkuu wa kwanza wa Israel kushtakiwa kwa uhalifu.

Wakati huo huo, ujumbe wa Israel uliokuwa Doha nchini Qatar wikendi iliyopita kwa mazungumzo ya awamu ya pili ya amani kwa Gaza unarejea kutoka nchini humo. Haya yamesemwa leo na msemaji wa Netanyahu bila ya kutoa maelezo zaidi.