*Asema wamejipanga kuendelea kuwatumikia wananchi
*Awashangaa wanaohoji CCM kukaa madarakani muda mrefu
Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Tanzania Bara Stephen Wasira amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu Chama kitaendelea kushika dola kutokana na wingi wa kura za wananchi na si mtutu wa bunduki.
Wasira aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Busega mkoani Simiyu alipokuwa akielekea jijini Mwanza.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/0-19.jpg)
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, CCM tutashinda maana hakuna wa kupambana na sisi. Lengo letu ni kushika dola na dola hatuishiki kwa bunduki bali tunaishika kwa kura zinazopigwa na wana CCM na wasio wana CCM,” alisema Wasira
Akieleza zaidi kuhusu uimara wa CCM amesema Chama hicho ni muungano wa vyama vilivyoleta ukombozi katika nchi uliotokana na vyama vya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP).
“Kwa hiyo wanachama na viongozi wa Chama tunabeba maono ya vyama vilivyopita na sisi ndio tunaendeleza kazi ya uhuru na kuboresha maisha ya watu.
“Wako watu wengine wako Ulaya na wengine wako hapa kama ‘maajenti’ wao, wanasema CCM imekaa sana nami nawauliza tulivyodai uhuru tulisema tutakaa mpaka lini?
“Tulidai uhuru kwa sababu kuna ajenda ya kubadili maisha ya watu, na kubadili maisha ya watu hakuna mwisho kwa sababu maendeleo yanazaa matatizo mapya.
“Tunaendelea kujenga Tanzania yenye maendeleo kuondoa matatizo.Nataka kuwaambia Chama chetu ni kwa ajili ya kuwakomboa watu ambao hawana uwezo na hata wakipata matatizo hawawezi kuweka wakili, hivyo CCM ndio wakili wao.
“Tunataka Chama hiki kiwe wakili wa watu wote, tuwe tumaini la makundi yote, tunataka liwe tumaini la vijana wa Tanzania, tunataka liwe tumaini la wafanyabiashara, tumaini kwa mama lishe, wamachinga.
Kwa mujibu wa Wasira, CCM ni chama cha wanachi na kuanzia sasa muda mwingi utatumika kuzungumza mambo ya watu.
“Tunataka kutumia muda zaidi kuzungumza mambo yanayohusu watu.Tunataka kujua watu wana matatizo gani na vikao vyetu vizungumze matatizo ya watu na kutatua kero,”alisema Wasira
Akifafanua zaidi alisema hata muundo wa mfumo uliopo unataka Chama Cha Mapinduzi kiwe daraja kati ya watu na Serikali ili Chama kijue matatizo ya watu na kimalize yanayowezekana na yanayohitaji dola aagizwe mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya kuhakikisha ufumbuzi wake.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/0-20.jpg)
“CCM ni wakala wa watu hivyo tuhakikishe dhuluma hailelewi katika maeneo yetu, Chama
chetu kilipoanza miaka 48 mimi nilikuwa mjumbe katika mkutano ulioanzisha CCM.
“Tulikubaliana kuunda chama chenye nguvu kimuundo na fikra ili kiwakomboe watu wanaohitaji ukombozi, watu ambao hawawezi kuajiri wakili. Chama hiki kiwe wakili wao na hiyo ndio kazi tunayoifanya katika ngazi ya Shina hadi Halmashauri Kuu ya Taifa,”aliongeza.
Hivyo, Wasira alisisitiza viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wazungumze mambo yanayohusu maslahi ya watu.
Kuhusu wagombea ndani ya Chama hicho alisema tayari wameshapata wagombea wao wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, hivyo wanawasubiria watani zao(wapinzani)na kwa hali ilivyo katika vyama vyao Ikulu wataiona kwenye luninga.
“Mpaka hivi ninaposimama hapa hakijapatikana chama mbadala wa kupambana na CCM hata CHADEMA imebakia nusu halafu watushinde. CCM ushindi ni lazima na ushindi unaotokana na kura.”