Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bahi
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Muhammed Mchengerwa ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kujitokeza kupambania tuzo mbalimbali zinazotolewa, kwani ni fursa inayowatambulisha ufanisi kwenye umma na inaimarisha utendaji wa kazi zao.
Alitoa wito huo wakati akikabidhi tuzo kwa waandishi wa habari mahiri 15 kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Pwani, Singida na Dodoma, kupitia mradi wa Shule Bora, unaotekelezwa kwa msaada wa Serikali ya Uingereza (UKaid) ikishirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),katika viwanja vya Shule ya Bahi English Medium Pre and Primary School (BEMPS) mkoani Dodoma.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002481813.jpg)
Miongoni mwa waandishi hao ni pamoja na Mwamvua Mwinyi kutoka Uhuru Media Group (UMG) na Blogs, Emmanuel Kapandila ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Halmashauri ya Rufiji, aliyeshinda katika kipengele cha maofisa habari wa Serikali, na Futuna Suleiman kutoka ITV.
“Tunawapongeza kwani wamefanikiwa kuandika na kuujulisha umma kuhusu shughuli za kielimu zinazotekelezwa na Mradi wa Shule Bora, ambapo kiasi cha sh. milioni 26 zimetolewa kwa waandishi hawa 15 sambamba na Tuzo kwa juhudi zao,” alifafanua Mchengerwa.
Mchengerwa aliwasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuandika habari zenye manufaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kuepuka kuandika habari zisizo na manufaa ambazo zinaweza kusababisha madhara katika jamii.
Akizungumzia kuhusu Mradi wa Shule Bora, Mchengerwa alisema ,tarehe 4 Aprili 2022, Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza, ilizindua mpango wa elimu bunifu wa Shule Bora wenye thamani ya Sh. bilioni 271, utakaosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, ujumuishi, na usalama kwa wasichana na wavulana katika shule za msingi nchini.
Anaeleza, Mradi huu unaotekelezwa kwa msaada wa Serikali ya Uingereza (UKaid), unashirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), katika mikoa tisa ya Tanzania Bara, ikiwemo Pwani, Tanga, Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu, Mara, na Rukwa.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002481814.jpg)
Mchengerwa alieleza kuwa tangu mwaka 2022 hadi kufikia 2024, mradi huu umejikita kuboresha elimu ngazi ya awali na msingi katika maeneo manne, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu, ufundishaji, ujumuishi, na uimarishaji wa mifumo ya mafunzo kwa walimu 4,944 katika halmashauri 19 za mikoa saba ya mradi huu.
Aidha walimu 6,937 walipata mafunzo ya namna ya kuibua hadithi za kujifunza na ufundishaji ili kuboresha ufundishaji katika halmashauri 29.
Vilevile, walimu 1,747 wa awali na wa darasa la kwanza na la pili, wawezeshaji rika, na viongozi wa shule kutoka mikoa ya Pwani, Simiyu, Rukwa, Mara, Dodoma, na Tanga walipata mafunzo hayo.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002481815.jpg)