Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
Wakazi wa Kijiji cha Image kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, wametakiwa kuacha tabia ya kutunza fedha nyumbani badala yake watumie huduma za kibenki ili kuepuka uharibifu wa fedha na vitendo vya wizi na uporaji baada ya wezi kubaini uwepo wa fedha majumbani.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Muhogofya Mfalamagoa wakati akizungumza na wananachi wa Image siku NMB Kijiji Day iliyofanyika kijijini hapo.
Amesema wamefika kwa lengo la kutoa elimu ya fedha kwa kuwa wananchi wamekuwa na uchumi mkubwa lakini wameshindwa kuhifadhi fedha kwenye mazingira sahihi.
Amesisitiza kuwa,” Sio jambo jema kuhifadhi fedha nyumbani kwa kuwa ni hatarishi na unaweza kupoteza fedha zako pamoja na kupoteza maisha yako kwa kuwa watu wakijua una fedha watakuja kuiba na huwezi kujua watakuacha katika hali gani kwa hiyo ni muhimu sana kuweka benki ndio maana pia tumekuja na bidhaa ya NMB pesa account ambayo tunaifungua kwa shilingi elfu moja tu,” amesema.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Njombe, Daniel Rauya amesema maudhui ya kijiji day ni kuwasogezea huduma wananchi vijijini.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Dk. Frank Mganga ambaye pia Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo amepongeza zoezi hilo lililozaa matunda kwa kuwa wananchi wanauhitaji mkubwa wa huduma za kibenki.
Mwenyekiti wa kijiji cha Image, Felix Payovela ameishukuru benki ya NMB kwa kuwafikia wakazi wa kijiji hicho na kuwaingiza kwenye mfumo wa kibenki ambapo amesema kwa sasa wananchi watakuwa wakitunza fedha zao sehemu salama.
Nao baadhi ya wananchi wa Image akiwemo Moses Kuchogola wameshukuru benki hiyo kwa kuwafikia na kuwapa elimu kwa kuwa awali walikuwa wakihifadhi fedha katika mazingira yasiyo salama.
Licha ya wananchi wa maeneo hayo kujitokeza na kufungua akaunti hata hivyo wapo waliojitokeza na kuhitaji uwakala katika siku hiyo ambayo imeadhimishwa kwa kufanyika matukio mbalimbali ikiwemo mazoezi ya kukimbia (Joging) michezo ya mpira wa miguu, kuvuta kamba, kufukuza kuku pamoja kwenye gunia.